Mvua yazima ndoto za Mkenya Jumuiya ya Madola

GLASGOW: BINGWA mtetezi wa mbio za mita 100 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola Mkenya, Ferdinand Omanyala, amesema hali mbaya ya hewa iliyotawaliwa na mvua na baridi kali jijini Glasgow ndiyo iliyochangia kushindwa kwake kutetea taji alilolitwaa mwaka 2022.
Omanyala alisema hakuwa katika kiwango chake kutokana na mvua iliyonyesha wakati wa mbio za nusu fainali, akieleza kuwa siku zote amekuwa akipata ugumu wa kukimbia kwenye mvua.
Bingwa huyo katika mashindano hayo alimaliza nafasi ya sita katika nusu fainali ya pili kwa kutumia sekunde 10.19, hivyo kushindwa kutinga fainali na kupoteza ndoto ya kutwaa ubingwa wa pili mfululizo.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 30 alikuwa akilenga kuongeza taji jingine la kimataifa baada ya kutwaa dhahabu katika mashindano ya jumuhia ya madola yaliyofanyika Birmingham miaka minne iliyopita. Hata hivyo, matumaini hayo yalifutwa na hali mbaya ya hewa iliyotawala uwanja wa mashindano.
Usiku huo ulimwangukia nyota mwanariadha wa Cameroon, Emmanuel Esseme, aliyeng’ara kwa kutumia sekunde 9.83 na kutwaa medali ya dhahabu ya mita 100, akiendeleza mafanikio yake makubwa ya msimu huu.
Licha ya maumivu ya kushindwa, Omanyala alisema anafurahishwa na maendeleo makubwa ya wanariadha wa mbio fupi barani Afrika, akieleza kuwa ushindani unaongezeka na kizazi kipya kinaendelea kung’ara kimataifa.
Mkenya huyo pia alikiri kuwa msimu huu ulianza vizuri baada ya kurejea katika kiwango chake, akifanikiwa kukimbia chini ya sekunde 10 mara tano kati ya Aprili na Mei, huku ushindi wake katika mbio za Diamond League mjini Xiamen kwa muda wa sekunde 9.94 ukiwa moja ya mafanikio makubwa.
Omanyala amesema kushindwa mashindanoni ni pigo kubwa, lakini anaamini bado ana nafasi ya kujirekebisha kuelekea Mashindano ya Dunia ya Riadha yatakayofanyika mwakani mjini Beijing, sambamba na kuendelea kushiriki mbio za Diamond League zinazotarajiwa kumpa nafasi ya kurejea kwenye jukwaa la ushindi.




