
BRAZIL: FAMILIA ya mwanariadha wa mbio za marathon wa Brazil, Daniel Ferreira do Nascimento, imetoa wito wa dharura kwa umma kusaidia kufanikisha juhudi za kumpata baada ya kutoweka bila kujulikana aliko.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Daniel alionekana kwa mara ya mwisho Juni 19, mwaka huu, akiondoka nyumbani kwake mjini Paraguaçu Paulista, jimbo la São Paulo, akiwa amebeba mkoba mweusi pekee.
Mama yake amesema mwanaye alikuwa akipitia kipindi kigumu cha maisha baada ya kufungiwa kushiriki mashindano ya riadha kwa muda mrefu kutokana na adhabu aliyokumbana nayo, hali ambayo ilimwathiri kisaikolojia.
Jeshi la Polisi nchini Brazil limeanza uchunguzi wa kutoweka kwa mwanariadha huyo huku likiendelea kukusanya taarifa kutoka kwa wananchi na watu waliokuwa karibu naye ili kubaini alipo.
Daniel aliwahi kuiwakilisha Brazil katika mbio za marathon za Michezo ya Olimpiki na alikuwa miongoni mwa wanariadha waliokuwa wakitarajiwa kufanya vizuri kabla ya taaluma yake kukumbwa na changamoto zilizotokana na adhabu ya kufungiwa kushiriki riadha.




