Drake apoteza dola 300,000 mechi ya Argentina, Canada

MWANAMUZIKI nyota wa Canada, Drake amepoteza dola za Marekani 300,000 alizoweka kama dau kwenye mchezo wa kubeti baada ya timu yao ya taifa kufungwa na Argentina katika mechi ya nusu fainali ya mashindano ya Copa America.
Drake aliweka fedha hizo na alikuwa akitarajia kupata kiasi kikubwa cha fedha ambazo ni zaidi ya dola za marekani 2,880,000 kama Canada ingeifunga Argentina inayoongozwa na Messi ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la dunia lakini wakafungwa 2-0.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa MetLife mjini New York, Mabao ya Lionel Messi na Julián Álvarez wa Manchester City yaliwahakikishia Argentina kutinga fainali ya mchezo huo.
Mapema Jumanne mchana, Drake akishiriki karatasi yake ya dau kwenye Instagram aliandika: “Hii inaweza kumpata Messi @stake.”
Argentina sasa itachuana na mshindi wa leo wa nusu fainali kati ya Uruguay na Colombia kwenye fainali itakayopigwa Uwanja wa Hard Rock huko Miami Gardens, Florida siku ya Jumapili, Julai 14 mwaka huu.




