Habari Mpya

PM aibana TFF, sakata la viwanja vibovu

DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF kutoa masharti kwa klabu zinazomiliki viwanja kufuata maelekezo na wasiotimiza wawekwe pembeni

Waziri mkuu Majaliwa ametoa maagizo hayo katika hafla ya uzinduzi wa mtambo wa teknolojia ya usaidizi wa muamuzi kwa njia ya video VAR shughuli iliyoandaliwa na kampuni ya azam media katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Amesema soka la Tanzania limekuwa na muendelezo mzuri kwa sababu ya maboresho ya miundombinu kwa sekta zote ikiwemo Azam Media kuleta mitambo ya kisasa itakayosaidia kupeleka soka la Tanzania duniani.

“Kazi iliyopo TFF kuwapa masharti wanachama wao wanaomiliki viwanja asiyetimiza awekwe pembeni, mkae na Azam media pamoja na wachumi ili kuingia mkataba kwa ajili ya kufanya biashara na sio siasa.

Tunahitaji kufika mbali kwenye viwango vya Afrika baada ya namba sita basi tuwe hadi namba nne, tatu hata mbili tukapambane na Morocco na Misri,” amesema Waziri mkuu Majaliwa.

Amesema kutokana na Serikali kuipa kipaumbele michezo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan ameingia mwenyewe katika michezo na kuondoa ile dhana ya Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu.

“Anahamasisha michezo kwa kutoa motisha, mfano lile goli la mama kwa timu za taifa hata klabu ambazo zitashiriki michuano ya kimataifa. Pia kuwa wenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON ) 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda,” amesema Majaliwa.

Ameongeza kuwa maboresho ya uwanja ikiwemo miundo mbinu ambayo kuwepo kwa viti vya mashabiki, Taa za uwanjani pamoja na sehemu ya kuchezea yenye kukidhi matakwa ya TFF na Bodi ya ligi.

“Hii VAR inatusaidia kuondoa malalamiko kwa timu pamoja na kupunguza makosa ya kibinadamu kwa waamuzi wetu na kuwa makini katika kazi zao,” aliongeza

Waziri mkuu Majaliwa ameuambia umma wa watanzania kuwa Serikali itatimiza ahadi yake ya kuongeza set nyingine ya VAR nchini.

Related Articles

Back to top button