Ligi Kuu

Azam, Simba kwenye vita leo

DAR ES SALAAM: AZAM FC leo inamkaribisha Simba katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, kuanzia saa 1:00 usiku, katika mchezo unaotarajiwa kuwa mtihani mkubwa kwa safu za ulinzi za timu hizo kutokana na uwezo wao wa kufumania nyavu msimu huu.

Uwezo wa Azam na Simba kufunga mabao katika Ligi Kuu sambamba na historia ya kukutana kwao hivi karibuni, unaifanya mechi hiyo kuwa miongoni mwa mechi zinazotarajiwa kuwa na ushindani.

Azam imecheza mechi sita hadi sasa, ikishinda nne na kutoka sare mbili, huku ikifunga mabao 11 na kuruhusu matano. Simba kwa upande wake imecheza michezo mitano na kushinda yote, ikiwa imefunga mabao tisa na kufungwa mawili pekee.

Takwimu hizo zinaonesha ubora wa timu zote mbili katika safu za ushambuliaji, huku Simba ikiwa na rekodi ya asilimia 100 ya ushindi katika mechi zake tano za kwanza za ligi msimu huu.

Historia ya mechi zao imekuwa ikionesha ushindani wa karibu. Katika mechi 10 za mwisho za Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba imeshinda tatu, Azam imeibuka na ushindi mara mbili, huku michezo mitano ikimalizika kwa sare.

Wachezaji hatari ni Abdul Sopu wa Azam FC aliyefunga mabao manne kati ya 11 ya timu hiyo na kuwa kinara wao wa ufungaji hadi sasa huku Libasse Gueye, kwa upande wa Simba akihusika katika mabao sita kati ya tisa ya timu hiyo akiwa amefunga moja na kutoa pasi tano za mwisho.

Related Articles

Back to top button