Ligi Kuu

Yanga ina mtihani mgumu mbele ya Geita leo

DAR ES SALAAM: MABINGWA wa Tanzania, YANGA  leo itakuwa na kazi ya kuendeleza mwanzo mzuri wa msimu, lakini safari hii ikikabiliwa na mtihani wa uchovu dhidi ya Geita Gold katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex kuanzia saa 1:00 usiku.

Yanga inaingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kucheza mechi ngumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana Jumamosi, ambayo iliifunga mabao 2-1 na kutinga raundi ya pili ya awali kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2.

Ushindi huo umeifanya timu hiyo kuendelea na kampeni zake za kimataifa, huku ikiwa na mchezo mwingine wa CAF dhidi ya CFFA ya Madagascar unaosubiri mbele.

Hivyo, kocha Manqoba Mngqithi anakabiliwa na jukumu la kuhakikisha kikosi chake kinaendelea na kasi katika ligi bila kuathiriwa na mzigo wa mechi za kimataifa, hasa kwa kuzingatia muda mfupi uliopo kati ya mchezo wa Gaborone United na wa leo.

Yanga inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 15 baada ya kushinda michezo yote mitano iliyocheza, huku ikiwa imefunga mabao 15 na kuruhusu mawili pekee. Geita Gold yenyewe ina pointi saba katika michezo mitano, ikiwa imeshinda miwili, sare moja na kupoteza miwili.

Pamoja na tofauti hiyo ya viwango, Geita Gold si timu ya kubezwa kutokana na namna ilivyoanza msimu huu. Ushindi wa mabao 6-2 dhidi ya Kagera Sugar pamoja na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam FC unaonesha kuwa timu hiyo ina uwezo wa kutumia udhaifu wa wapinzani wake, jambo ambalo Yanga inapaswa kulizingatia.

Historia pia ipo upande wa mabingwa hao watetezi, ambao wameifunga Geita Gold katika michezo yote saba iliyopita tangu mwaka 2021. Katika michezo hiyo, Yanga imefunga mabao 11 huku Geita Gold ikifunga bao moja pekee.

Hata hivyo, historia hiyo haitoshi kumpa Yanga ushindi wa leo kwani changamoto kubwa ipo katika namna itakavyoweza kuhimili baada ya kutumia nguvu nyingi kwenye pambano la kimataifa. Geita Gold nayo inaingia uwanjani ikiwa haina presha kubwa, ikitafuta kuandika historia mpya dhidi ya mabingwa hao.

Related Articles

Back to top button