Kwingineko

Hispania yatoa neno kuhusu fainali

....Lamine Yamal, Porro wako 'fiti'

MAREKANI: Timu ya taifa ya Hispania imepata afueni kuelekea fainali ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Argentina baada ya kuthibitisha kuwa nyota wake Lamine Yamal na Pedro Porro wanatarajiwa kuwa fiti kwa mchezo huo, licha ya kufanya mazoezi tofauti na wenzao Alhamisi.

Yamal na Porro walifanya mazoezi maalumu katika moja ya viwanja vya mazoezi vya Red Bull New York, New Jersey, wakati kikosi kingine kikianza maandalizi rasmi ya mchezo wa fainali utakaochezwa Jumapili.

Hatua hiyo ilizua wasiwasi kuhusu hali zao za kiafya, lakini Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) limesema ni sehemu ya mpango wa kudhibiti mzigo wa mazoezi na kuwahifadhi wachezaji hao kwa ajili ya mechi hiyo muhimu.

Kocha Luis de la Fuente alieleza baada ya ushindi wa Hispania dhidi ya Ufaransa katika nusu fainali kuwa beki Pedro Porro alikuwa akisumbuliwa na maumivu madogo. Taarifa zinaeleza kuwa ana tatizo la misuli ya nyuma ya paja, lakini hali hiyo haionekani kuwa mbaya kiasi cha kumuweka nje ya fainali.

Kwa upande wa Lamine Yamal, hali yake inaonekana kuwa nzuri zaidi. Kocha De la Fuente alisema baada ya mchezo dhidi ya Ufaransa kuwa mshambuliaji huyo kijana hakuwa na majeraha makubwa, ingawa alibaki na maumivu ya kawaida na michubuko kutokana na mapambano makali aliyokutana nayo dhidi ya mabeki Lucas Digne na Theo Hernandez.

Katika dakika 15 za mazoezi zilizoruhusiwa kushuhudiwa na vyombo vya habari, wachezaji wengine wa Hispania walionekana wenye ari na utulivu licha ya kukabiliwa na hali ya hewa ya joto na unyevunyevu wa takribani nyuzi 30 za Selsiasi.

Kikosi hicho kina siku tatu za kujiandaa na kuzoea mazingira kabla ya kuvaana na Argentina katika pambano la kuwania ubingwa wa dunia.

Hispania sasa inaweka nguvu zote kuhakikisha Yamal, Porro na wachezaji wengine wanaingia uwanjani wakiwa katika kiwango bora, wakilenga kutwaa taji la Kombe la Dunia mbele ya mabingwa watetezi Argentina.

Related Articles

Back to top button