Thierry Henry, Pele wapewa mitaa Marekani

NEW YORK: JIJI la New York limezindua heshima maalum kwa mastaa wawili wakubwa wa soka duniani kwa kubadilisha kwa muda majina ya baadhi ya mitaa na kuyapa majina ya Thierry Henry na Pele kuelekea kuanza rasmi kwa Kombe la Dunia 2026.
Hatua hiyo imekuja wakati dunia ikisubiri mashindano hayo makubwa yanayoandaliwa kwa pamoja na Marekani, Mexico na Canada kuanza rasmi, huku fainali ikitarajiwa kuchezwa mwezi ujao katika uwanja wa MetLife utakaotumika kwa jina la New York New Jersey Stadium.
Maelfu ya mashabiki walikusanyika eneo la West 50th Street na 6th Avenue katikati ya Manhattan kushuhudia uzinduzi wa barabara mpya iliyopewa jina la Thierry Henry Way ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa gwiji huyo katika soka la dunia.
Henry, aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Arsenal na Barcelona na mshindi wa Kombe la Dunia mwaka 1998 akiwa na Ufaransa, alishiriki hafla hiyo kupitia mawasiliano ya video.
Mbali na mafanikio yake Ulaya, Henry pia aliwahi kucheza kwa miaka mitano katika klabu ya New York Red Bulls kwenye Ligi Kuu ya Marekani (MLS), jambo lililomfanya kuwa mmoja wa wachezaji waliopata nafasi kubwa katika historia ya soka nchini humo.
Katika hatua nyingine, jiji hilo pia limebadili kwa muda jina la makutano ya Shea Road na Meridian Road katika eneo la Queens na kuyaita kwa jina la gwiji wa Brazil, Pele.
Majina hayo mapya ya mitaa yataendelea kutumika hadi Novemba 1 mwaka huu kama sehemu ya maadhimisho ya Kombe la Dunia na kutambua mchango wa magwiji hao katika kuikuza soka duniani.




