Jua Kali aahidi makubwa miaka 30 ya Bongo fleva

MSANII wa muziki kutoka Kenya, Paul Nunda maarufu kwa jina la Jua Kali, amewasili jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya maandalizi ya kushiriki Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva litakalofanyika kesho, Julai 10, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokelewa, Jua Kali ali amesema yuko tayari kuwapa mashabiki burudani ya kiwango cha juu na kufanya tamasha hilo kuwa la kukumbukwa.
Msanii huyo amesema hatarajii kufanya maonesho ya kawaida, bali amejiandaa kutoa burudani itakayowaacha na kumbukumbu nzuri mashabiki wake wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
“Kesho naenda kuua tu kama ni Kenya,” amesema Jua Kali, amesisitiza utayari wake wa kutumbuiza katika tamasha hilo linaloadhimisha miaka 30 ya muziki wa Bongo Fleva.
Kwa mujibu wa waandaaji wa tamasha hilo, tiketi zote zimekwishauzwa, hali inayoonyesha hamasa kubwa ya mashabiki kushuhudia maonesho hayo.
Waandaaji wamewataka wote waliokata tiketi kufika mapema ukumbini ili kuepuka usumbufu na kupata nafasi nzuri ya kufurahia burudani kutoka kwa nyota mbalimbali wa Bongo Fleva watakaopanda jukwaani katika maadhimisho hayo ya kihistoria.




