Isha Mashauzi arejea kuadhimisha miaka 20 ya muziki

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa taarabu nchini, Isha Ramadhan maarufu kama Isha Mashauzi, ametangaza kurejea rasmi kwenye anga la muziki baada ya ukimya wa muda, huku akipanga kufanya tamasha maalum mwezi Agosti mwaka huu kuadhimisha miaka 20 tangu aanze safari yake ya muziki.
Akizungumza na waandishi wa Habari Dar es Salaam jana Juni 10, Isha amesema alianza muziki wa taarabu mwaka 2006 na kwamba mwaka huu wa 2026 unatimia miongo miwili tangu aanze kuitumikia sanaa hiyo, jambo ambalo anaona linastahili kupewa heshima ya kipekee kupitia tamasha hilo.
“Nimeanza muziki mwaka 2006 na sasa tuko mwaka 2026. Hili si jambo la kuliacha lipite hivi hivi. Ninawaambia mashabiki wangu wote, ‘Queen is back’, malkia nimerudi,” amesema.
Msanii huyo amesema kwa muda mrefu amekuwa akipokea maswali kutoka kwa mashabiki wake wakitaka kufahamu sababu za kutotoa nyimbo mpya, hali iliyomfanya kuona ni wakati muafaka wa kurejea tena jukwaani.
Amesema katika kipindi hicho aliamua kupunguza shughuli za muziki na kujikita zaidi katika biashara zake binafsi, hususan biashara ya chakula, lakini sasa ameona ni wakati wa kurudi na kuendeleza mchango wake katika muziki wa taarabu.
“Katikati nilipumzika kidogo nikiendelea na biashara yangu ya chakula, lakini nimeamua kurudi baada ya kuona wale tuliowaachia wameshindwa kuendeleza muziki kwa kiwango tulichokuwa tunakitarajia,” amesema.
Isha amesema sehemu ya maandalizi ya tamasha hilo ni kuzindua wimbo wake mpya unaoitwa “Kacheze Unakochezaga”, ambao utakuwa miongoni mwa nyimbo atakazozitumbuiza siku ya tamasha hilo.
Kwa mujibu wa msanii huyo, tamasha la maadhimisho ya miaka 20 litakuwa fursa ya kukutana tena na mashabiki wake, kukumbuka historia ya safari yake ya muziki na kuonesha kuwa bado ana nafasi kubwa katika kuendeleza muziki wa taarabu nchini.




