Waamuzi watatu wasimamishwa mizunguko mitano

DAR ES SALAAM:WAAMUZI watatu wa Ligi Kuu wameondolewa kwenye orodha ya waamuzi kwa mizunguko mitano kutokana na mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyojitokeza katika michezo tofauti ya ligi.
Waamuzi hao ni Liston Hiari wa Dar es Salaam aliyechezesha mchezo kati ya Mbeya City FC na Mtibwa Sugar, pamoja na Hance Mabena wa Tanga na mwamuzi msaidizi Frank Komba waliohusika katika mchezo kati ya Simba SC na Pamba Jiji FC.
Kwa mujibu wa TPLB, waamuzi hao walionesha mapungufu yaliyotokana na kushindwa kutafsiri kwa usahihi sheria za mchezo wa mpira wa miguu.
Katika hatua nyingine, shabiki wa Yanga Said Selemani Ally, amefungiwa kuingia viwanjani kwa miezi 12 baada ya kuingia eneo la kuchezea na kumwaga kimiminika pamoja na udongo uwanjani kabla ya mchezo dhidi ya Mashujaa FC, kitendo kilichotafsiriwa kama imani za kishirikina.
Mbali na hilo, klabu ya Mapinduzi FC ya Mwanza imeadhibiwa vikali na TPLB baada ya kushindwa kufika kwenye mchezo wa First League dhidi ya Endument FC uliopaswa kuchezwa katika Uwanja wa BRN Complex mkoani Kilimanjaro.
Kutokana na kosa hilo, Endument FC imepewa ushindi wa mabao 3-0 na alama tatu, huku Mapinduzi FC ikitozwa faini ya Sh milioni mbili, kupokwa alama tatu kwenye msimamo wa ligi na kutakiwa kulipa gharama za maandalizi ya mchezo huo.
Aidha, Mwenyekiti wa Mapinduzi FC, Hemedi Msema, amefungiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na kushindwa kwa timu yake kufika uwanjani bila sababu za msingi.
Wakati huo huo, TPLB imemrejeshea haki ya kushiriki shughuli za mpira wa miguu mchezaji wa IAA, Joseph Ombeni, baada ya kupunguza adhabu yake ya kufungiwa miezi 12.
Ombeni alikuwa ametumikia miezi minne ya adhabu hiyo iliyotokana na ukiukwaji wa taratibu za usajili, na kamati imezingatia maombi yake pamoja na mafunzo aliyodai kuyapata wakati wa kifungo hicho.




