Aucho: Tulipoteza umakini

SINGIDA: KIUNGO wa Singida Black Stars, Khalid Aucho amesema kupoteza umakini katika dakika za mwisho kumeigharimu timu yake baada ya kufungwa mabao 2-1 na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Airtel.
Aucho amesema licha ya kupoteza mchezo huo, timu yao ilicheza vizuri na ilitengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo.
“Tumepoteza umakini katika dakika za mwisho na hilo limetugharimu.
Tulitengeneza nafasi nyingi lakini hatukuweza kuzitumia. Pia kulikuwa na baadhi ya maamuzi ambayo tulihisi tulistahili kupata, kama penalti, lakini haikuwa upande wetu. Hiyo ndiyo soka,” amesema Aucho.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Uganda amesema kwa upande wa kiwango cha uchezaji hawakuwa wabaya kwa kuwa walipambana na kutengeneza nafasi, jambo linaloonesha timu ilifanya kazi yake vizuri uwanjani.
“Kama unatengeneza nafasi nyingi maana yake unafanya kitu sahihi uwanjani, lakini tatizo letu lilikuwa kushindwa kuzimalizia. Hilo ndilo tunalopaswa kuboresha,” amesema.
Pia, amewaomba mashabiki wa Singida Black Stars kuwa na subira baada ya matokeo hayo, akiahidi kuwa katika mchezo ujao watajitahidi kufanya vizuri zaidi ili kuwafurahisha.
“Tunajua mashabiki hawajafurahishwa na matokeo ya leo, lakini tunawaahidi katika mchezo ujao tutafanya vizuri zaidi ili kuwafanya wafurahi,” amesema Aucho.




