Ligi Kuu

Simba, Mtibwa Sugar zatozwa milioni 15, ushirikina

DAR ES SALAAM :KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imezitoza faini Simba SC na Mtibwa Sugar jumla sh milioni 15 kutokana na makosa tofauti yaliyobainika katika michezo ya Ligi Kuu.

Mtibwa Sugar imetozwa faini ya Sh milioni tano baada ya wachezaji wake pamoja na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi kuonekana wakifanya vitendo vilivyotafsiriwa kuashiria imani za kishirikina kabla ya mchezo dhidi ya Mbeya City FC.

Kwa mujibu wa TPLB, kundi hilo lilijikusanya katikati ya uwanja likiomba dua huku mmoja wa viongozi akionekana kuchimbia vitu ardhini.

Katika hatua nyingine, Simba SC imepigwa faini ya Sh milioni 10 baada ya mashabiki wake kumwagia maji mwamuzi msaidizi namba moja wakipinga maamuzi yake wakati wa mchezo dhidi ya Pamba Jiji FC.

Kamati hiyo imeeleza kuwa hilo ni kosa la kujirudia kwa mashabiki wa Simba ndani ya msimu huu. Na katika hatua nyingine, Pamba Jiji imetozwa faini ya Sh 500,000 baada ya wachezaji wake sita kuoneshwa kadi za njano katika mchezo huo.

 

Related Articles

Back to top button