Serengeti Girls yajipanga kwa nusu fainali Cecafa

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa Serengeti Girls, Esther Chabruma, amesema kikosi chake kitarejea mazoezini kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Kenya kabla ya mchezo ujao wa nusu fainali.
Katika mchezo wa hatua ya makundi wa michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam, licha ya sare timu zote mbili zimetinga hatua ya nusu fainali baada ya kushinda kila mmoja mchezo mmoja na kutoka sare moja.
Akizungumza na SpotiLeo baada ya mchezo huo, Chabruma amesema mechi ilikuwa ngumu na ya ushindani mkubwa huku pande zote mbili zikishambuliana mara kwa mara.
“Mchezo ulikuwa mzuri kwa pande zote mbili. Tulishambuliana kwa wakati na sisi tulipata bao mapema, lakini makosa yaliyotokea ndiyo yamezaa bao la kusawazisha. Hata hivyo, hilo limeisha na sasa tunajipanga kwa ajili ya nusu fainali ili kufika fainali,” amesema Chabruma.
Amesema benchi la ufundi litaitumia muda uliobaki kurekebisha makosa yaliyoonekana kwenye mchezo huo ili timu iwe katika kiwango bora zaidi kuelekea hatua inayofuata ya mashindano.
Kocha wa Kenya Mildred Cheche amesema wamekuwa wakitengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia hivyo, wanahitaji kujirekebisha yasitokee katika mchezo wa nusu fainali akisema michuano hiyo inampa nafasi ya kujitathmini na kujiandaa na michuano ya kufuzu Kombe la Dunia ambapo hivi karibuni watacheza na Afrika Kusini baada ya kumalizika kwa Cecafa.




