Bandari, Rhino Rangers vita ya ubingwa wa First Ligi

DAR ES SALAAM: HATIMAYE bingwa wa Ligi Daraja la pili (First League) atafahamika leo wakati Bandari Tanzania ikishuka dimbani kuivaa Rhino Rangers katika mchezo wa fainali utakaopigwa saa 1:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Timu zote mbili zinaingia kwenye mchezo huo zikiwa na morali kubwa baada ya kufanya vizuri msimu mzima na kufanikiwa kutimiza malengo yao ya kupanda Ligi ya Championship.
Kocha Mkuu wa Bandari Tanzania, Omega Seme, amesema kikosi chake kipo tayari kwa pambano hilo na kinaingia uwanjani kikiwa na lengo la kutwaa ubingwa.
“Sisi kama timu tumejiandaa vizuri kupambana, wachezaji wako tayari. Naamini mchezo utakuwa mzuri na tumejiandaa kupata ushindi.
Tunahitaji mashabiki wa Bandari wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono,” amesema Seme.
Kwa upande wa Rhino Rangers, Kocha Mkuu Gifts Emanuel amesema hawana presha yoyote kuelekea fainali hiyo kwa kuwa tayari wamefanikiwa kupata tiketi ya kupanda Championship.
Emanuel amesema malengo yao sasa ni kumaliza msimu kwa kutwaa ubingwa ili kuweka historia na kuendeleza mwendo mzuri waliouonesha tangu mwanzo wa msimu.
“Hatuna presha kwa sababu tayari tumeshapanda Championship. Tunachotaka ni kutengeneza historia kwa kuwa mabingwa wa First League ili tuwe na mwendelezo mzuri kama tulivyokuwa tunatafuta kuingia Championship. Timu imejiandaa vizuri kisaikolojia na kimwili, tumewafundisha mbinu za kucheza fainali,” amesema Emanuel.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ubora uliooneshwa na timu hizo mbili msimu huu, huku kila mmoja ukisaka kumaliza kampeni zake kwa kunyanyua taji la First League.




