Simba yaitafuta Yanga kwa Pacome
DAR ES SALAAM: MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ameendelea kupiga kwenye mshono kwa Yanga kwa kudai kuwa wanamuanglia Pacome Zouzoua kwa uchu.
Amesema licha ya kuhitaji huduma ya kiungo huyo, wao hawakurupuki bali watatuma mtaalamu kutoka benchi la ufundi anayehusika kufuatilia viwango vya wachezaji kabla ya kuwasajili.
Ikumbukwe kuwa mkataba wa Pacome upo ukingoni na yupo kwenye mazungumzo na mabosi wake wa Yanga kuhusu kuongezewa dau la usajili na mshahara.
Ahmed amesema wanaangalia kiwango cha Pacome na kikiwaridhisha watahangaika naye ila akiendelea kucheza kama alivyocheza mechi na Azam FC, watasitisha mpango wa kuvunja benki kumsajili.
“Akiendelea na kiwango alichocheza katika mechi mbili zilizopita tutawaachia kama ilivyo kwa Chama (Clatous) na Aziz Ki (Stephen) ambaye tulikuwa na mpango naye lakini tukafanya tathimini ya kiwango chake tukamuacha,” amesema Ahmed.