Ligi Kuu

Barker: Hatuwadharau Mbeya City

MBEYA:KOCHA Mkuu wa Simba, Steven Barker, amesema kikosi chake hakitawadharau Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akieleza kuwa mechi za mwisho wa msimu huwa ngumu kutokana na kila timu kupambana kutimiza malengo yake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Mbeya kuelekea mchezo wa kesho utakaochezwa saa nane mchana, Barker amesema Mbeya City ni timu inayopigania kusalia ligi kuu, jambo linalofanya mchezo huo kuwa na ushindani mkubwa licha ya tofauti ya nafasi za timu hizo kwenye msimamo.

“Hatuwadharau wapinzani wetu. Kila timu kwa sasa ina malengo yake na unapocheza dhidi ya timu inayopambania kubaki ligi kuu, unapaswa kuwa makini zaidi kwa sababu mechi inakuwa ngumu,” amesema.

Kwa upande wake, beki wa Simba, David Kameta ‘Duchu’, amesema wachezaji wote wa timu hiyo wanafahamu wajibu wao katika kipindi hiki muhimu cha msimu na wako tayari kupambana kutafuta matokeo mazuri.

Wakati Simba ikisisitiza tahadhari, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga, amesema kikosi chake kipo katika mazingira magumu kutokana na vita ya kuepuka kushuka daraja, lakini kimejipanga vizuri kukabiliana na wapinzani wao.

Mayanga amdsema anatarajia mchezo wenye ushindani mkubwa kutokana na kukutana na timu inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi huku Mbeya City ikiwa katika kundi la timu zinazopambana kujinasua kutoka mkiani.

“Tumejiandaa kupambana nao kiufundi na kimbinu. Tunajua ubora wa Simba lakini sisi pia tunahitaji pointi kwa ajili ya kutimiza malengo yetu,” amesema Mayanga.

Naye mshambuliaji wa Mbeya City, Eliud Ambokile, amesema mchezo huo hautakuwa rahisi kwa kuwa kila upande una jambo muhimu la kupigania.

“Sisi tunapambana tusishuke daraja na wao wanapambana kuchukua ubingwa wa ligi, hivyo kila timu itapambana kwa nguvu zote kutafuta ushindi,” amesema Ambokile.

Related Articles

Back to top button