NBCPL kitapigwa New Amaan complex
DAR ES SALAAM: SIMBA na Yanga mmesikia?. Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TBPL), Almas Kasongo amesema kwenye kanuni mpya za 2024/25 timu za Bara ruhusa kutumia uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar kama uwanja wa nyumbani.
Kauli ya Ofisa Mtendaji huyo wa bodi ya ligi kuu inakuja wakati huu ambao ligi kuu Tanzania bara inatarajia kuanza siku 10 zijazo.
Kasongo amesema msimu uliopita walipokea barua kutoka klabu ya Simba kuomba kutumia uwanja wa New Amaan Complex ilishindikana kwa sababu ya kanuni ilieleza ligi hiyo kucheza Bara pekee.
“Msimu mpya wa 2024/25 tumekuja na kanuni mpya ikiwemo kuruhusu klabu au timu inayohitaji na kuamua kutumia uwanja wa New Amaan Complex, Visiwani Zanzibar, nimepokea barua kutoka timu moja katika ya 16 kuomba kutumia uwanja huo,” amesema Kasongo.
Licha ya Ofisa Mtendaji Kuu wa Bodi, kutoweka wazi ni timu ipi iliyopeleka barua, Spotileo imepenyezewa kuwa Simba wanahitaji kutumia uwanja wa New Amaan Complex baada ya uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam kufanyiwa ukarabati na Azam Complex uliopo Chamazi kutumiwa na Azam FC na Yanga.