Ligi Kuu

Julio: Mashujaa hatutafungwa na Yanga kirahisi

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Mashujaa FC, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, amesema hana hofu ya kuikabili Yanga akieleza kuwa ana uzoefu mkubwa dhidi ya mabingwa hao na anaamini si kazi rahisi kwake kufungwa na timu hiyo.

Akizungumza kuelekea mchezo wa Ligi Kuu utakaowakutanisha Mashujaa na Yanga Jumamosi, Julio amesema amewahi kupata ushindi dhidi ya Yanga akiwa kwenye timu tofauti na hivyo anaingia kwenye mchezo huo akiwa na kujiamini kwa kiwango kikubwa.

“Kwa mimi kufungwa na Yanga si kazi rahisi kwa sababu si timu ngeni kwangu, nawajua vizuri. Nikiwa Simba kama kocha niliwafunga, nikiwa Mwadui pia nimeshawafunga. Nafikiri hata wao wanajua wanaenda kucheza na kocha ambaye anajiamini,” amesema Julio.

Kocha huyo amesema kiwango cha kujiamini alichokuwa nacho wakati akiifundisha Simba ndicho anachokibeba hadi sasa akiwa Mashujaa, huku akisisitiza kuwa hana sababu ya kuingiwa na presha na mchezo huo.

Julio ameenda mbali zaidi kwa kulinganisha uwezo wa timu mbili kubwa nchini akidai kuwa kwa mtazamo wake Simba ina safu ya ushambuliaji iliyo bora zaidi kuliko Yanga.

“Naweza kusema Simba wanaweza kuwa na safu bora ya ushambuliaji kuliko Yanga. Kwangu Yanga ni timu nyepesi kwa jinsi wanavyocheza, lakini nawapa heshima zao kwa sababu wana wachezaji wazuri kama Prince Dube na Allan Okello,” amesema.

Hata hivyo, Julio amefichua kuwa tayari amezibaini silaha kuu za Yanga lakini hakutaka kuziweka wazi.

“Yanga wana silaha tatu, siwezi kuzitaja kwa sasa maana nitakuwa nimeuza siri za mchezo. Tumejipanga vizuri na tunajua nini cha kufanya,”amesema.

 

Related Articles

Back to top button