Kwingineko

MEXICO:KWA wengi ilikuwa ni bao la kawaida katika Kombe la Dunia. Lakini kwa Raúl Jiménez, lilikuwa moja ya nyakati kubwa zaidi katika maisha yake.

Miaka sita iliyopita, Jiménez alikuwa karibu kupoteza kila kitu baada ya kupata jeraha baya la kichwa katika mchezo wa Ligi Kuu England kati ya Arsenal na Wolverhampton Wanderers.

Katika tukio hilo, aligongana kwa nguvu na David Luiz na kupoteza fahamu akiwa uwanjani. Baadaye ilibainika kuwa alikuwa amepata ufa kwenye fuvu la kichwa pamoja na damu kuvuja ndani ya ubongo wake.Madaktari walilazimika kufanya upasuaji wa haraka ili kuokoa maisha yake.

Akikumbuka kipindi hicho, Jiménez aliwahi kusema kuwa madaktari walimweleza wazi jinsi hali yake ilivyokuwa hatari.

“Waliniambia ilikuwa miujiza mimi kuendelea kuwa hai. Fuvu la kichwa lilikuwa limepasuka na kulikuwa na damu ndani ya ubongo wangu. Ndiyo maana upasuaji ulipaswa kufanyika haraka,” amesema Jiménez.

Baada ya tukio hilo, alikaa nje ya uwanja kwa karibu miezi tisa akipambana kurejea katika hali yake ya kawaida.

Aliporudi kucheza soka, alilazimika kuvaa kinga maalum kichwani, kitu ambacho kimeendelea kuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku uwanjani.

Leo, miaka sita baada ya tukio hilo la kutisha, Jiménez ameandika ukurasa mwingine wa historia kwa kufunga bao lake la kwanza katika Kombe la Dunia mbele ya mashabiki wa Mexico kwenye Uwanja wa Azteca.

Ikumbukwe pia miezi mitatu tu iliyopita, Jiménez alipata pigo jingine kubwa baada ya kumpoteza baba yake aliyefariki dunia kutokana na ugonjwa wa saratani. Kifo hicho kilimuumiza sana mshambuliaji huyo ambaye mara nyingi amekuwa akizungumza kuhusu nafasi kubwa aliyokuwa nayo baba yake katika safari yake ya soka.

Sasa,baada ya mpira kuingia wavuni, hisia zilimzidi nguvu na machozi yakaanza kumtoka.Yalikuwa machozi ya mtu aliyewahi kuambiwa kuwa amenusurika kimiujiza baada ya jeraha la kutishia maisha,machozi ya mwana ambaye bado anaishi na majonzi ya kumpoteza baba yake miezi michache iliyopita.

Related Articles

Back to top button