Straika wa Gabon aanguka ghorofani, afariki

HANGZHOU:MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Gabon aliyekuwa anakipiga katika klabu ya Zhejiang FC yenye makazi yake katika mji wa Hangzhou nchini China, Aaron Boupendza amefariki Dunia baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya 11 ya Apartment aliyokuwa akiishi mjini humo leo Jumatano.
Kupitia taarifa iliyochapishwa katika mtandao wa X shirikisho la soka nchini Gabon (Fegafoot) limethibitisha kifo cha Mshambuliaji huyo aliyewika katika Kombe la Mataifa ya Africa AFCON 2021 lililofanyika nchini Cameroon mwaka 2022.
“Kwa masikitiko makubwa tunasikitika kuondokewa na moja ya vijana wa kutegemewa wa taifa hili baada ya kuanguka kutoka Ghorofa ya 11 ya jengo alilokuwa akiishi nchini China ambako alikuwa akiitumikia Zhejiang FC”
“Akiwa na miaka 28 Boupendza anatuacha na kumbukumbu ya mshambuliaji bora sana aliyeacha alama kubwa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Africa makala iliyofanyika nchini Cameroon” -imesema taarifa hiyo.
Kando na shirikisho hilo Rais mteule wa Gabon Brice Oligui Nguema ametumia mtandao wa X kuipa pole familia ya Boupendza na wadau wa soka nchini humo akimtaja mchezaji huyo kama mshambuliaji aliyeliheshimisha taifa.
Televisheni ya taifa hilo Gabon 24 imesema bado hakijajulikana hasa ni nini kimefanya tukio hilo kutokea huku ikisema mamlaka ya mji wa Hangzhou zimeanza uchunguzi na ukweli halisi wa kifo hicho utawekwa hadharani.
Enzi za uhai wake mzaliwa huyo wa Moanda, alicheza klabu Bordeaux ya Ufaransa mwaka 2016, akitumia muda wake mwingi kwa mkopo katika vilabu vingine vya nchi hiyo. Mwaka 2020 alisajiliwa na Hatayspor ya Uturuki alikokuwa mfungaji bora wa Super Lig msimu 2020-21 kabla ya kuhamia Al Arabi, ambayo alishinda nayo Kombe la FA la Qatar, na Al Shabab kwenye Ligi ya Saudi Pro League. Baadaye alitimkia Spells nchini Marekani akiwa na FC Cincinnati kisha Rapid Bucharest ya Romania kabla ya kuhamia China mwezi Januari mwaka huu.