La Liga

Ushindi wa Perez kumrejesha Mourinho Real Madrid

MADRID:KLABU ya Real Madrid inatarajiwa kumtangaza rasmi Jose Mourinho kama kocha mkuu mpya baada ya rais wa klabu hiyo, Florentino Perez, kushinda uchaguzi wa urais na kuendelea kuiongoza miamba hiyo ya soka la Hispania.

Mourinho, mwenye umri wa miaka 63, alisaini mkataba wa miaka mitatu mwezi uliopita, lakini utekelezaji wake ulikuwa unategemea matokeo ya uchaguzi huo. Kufuatia ushindi wa Perez, njia sasa imefunguka kwa kocha huyo raia wa Ureno kurejea katika dimba la Santiago Bernabeu kwa mara nyingine.

Perez, mwenye umri wa miaka 79, alipata asilimia 65 ya kura na kuendelea kushikilia nafasi ya urais ambayo ameiongoza tangu mwaka 2009. Baada ya kutangazwa mshindi, kiongozi huyo aliahidi kuendelea kuifanya Real Madrid kuwa moja ya klabu zenye mafanikio makubwa duniani.

“Tumeshinda uchaguzi na tutaendelea kufanya kazi kwa ajili ya kushinda mataji. Nipo hapa kuilinda Real Madrid na kuhakikisha inaendelea kuwa klabu ya mafanikio,” alisema Perez.

Kiongozi huyo pia alisisitiza dhamira yake ya kuifikisha Real Madrid kwenye ubingwa wa 16 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akijivunia kuwa na uwanja bora duniani pamoja na kikosi chenye baadhi ya wachezaji bora zaidi katika mchezo huo.

Katika hotuba yake, Perez alimkaribisha Mourinho kwa mikono miwili, akimtaja kuwa mmoja wa makocha bora duniani na mtu mwenye mapenzi ya dhati kwa Real Madrid.

“Tunajivunia kumkaribisha tena mmoja wa makocha bora duniani, Madridista wa kweli, Jose Mourinho,” alisema.

Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza katika kipindi cha miaka 20 kupata mpinzani wa kweli, baada ya mfanyabiashara wa sekta ya nishati mbadala, Enrique Riquelme, kuwania nafasi hiyo. Hata hivyo, Perez alionesha ubabe kwa kupata kura 21,741 dhidi ya kura 11,814 za mpinzani wake.

Mourinho anarejea Madrid baada ya kuondoka Benfica, ambako alichukua mikoba ya ukocha Septemba mwaka jana na kuiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu ya Ureno.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Mourinho kuinoa Real Madrid baada ya kuhudumu kati ya mwaka 2010 na 2013. Katika kipindi chake cha kwanza, aliiongoza klabu hiyo kutwaa ubingwa wa La Liga, Kombe la Mfalme (Copa del Rey) na Spanish Super Cup.

Kocha huyo atachukua nafasi ya Alvaro Arbeloa, ambaye aliteuliwa Januari mwaka huu kufuatia kuondoka kwa Xabi Alonso. Hata hivyo, Arbeloa alishindwa kuirejesha Real Madrid katika njia ya mafanikio baada ya msimu wa 2025/26 kumalizika bila taji lolote.

Msimu huo ulimalizika kwa maumivu kwa mashabiki wa Madrid baada ya wapinzani wao wakubwa Barcelona kutwaa ubingwa wa La Liga, wakihitimisha safari hiyo kwa ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa El Clasico.

Sasa macho ya mashabiki wa Real Madrid yanaelekezwa kwa Mourinho, ambaye anatarajiwa kupewa jukumu la kurejesha hadhi ya klabu hiyo na kuiongoza katika harakati za kurejesha mataji ya ndani na kimataifa.

Related Articles

Back to top button