Kifaa kinachosaidia moyo wa Eriksen

DENMARK:WIKIENDI iliyopita, Christian Eriksen aliwapa hofu mashabiki wa soka duniani baada ya kuanguka uwanjani katika dakika ya 65 ya mchezo dhidi ya Ukraine, tukio ambalo liliwakumbusha wengi yaliyotokea wakati wa Euro 2020.
Baada ya Eriksen kuanguka, wachezaji wa timu zote mbili walikusanyika kumzunguka huku madaktari wakikimbilia kutoa huduma ya haraka. Kwa muda mfupi, hali hiyo ilirejesha kumbukumbu za tukio la miaka kadhaa iliyopita ambapo nyota huyo wa Denmark alipata mshtuko wa moyo akiwa uwanjani.
Hata hivyo, safari hii kulikuwa na tofauti kubwa.
Baada ya tukio la Euro 2020, Eriksen aliwekewa kifaa maalumu cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo. Kifaa hicho hufuatilia mapigo ya moyo muda wote na kina uwezo wa kugundua mabadiliko hatari yanayoweza kuhatarisha maisha.
Iwapo mapigo ya moyo yatakuwa katika hali hatari, kifaa hicho hutoa mshtuko wa umeme unaosaidia kurejesha mdundo wa kawaida wa moyo.
Daktari wa timu ya Denmark, Morten Boesen, amesema kifaa hicho kilifanya kazi kama kilivyopangwa.
“Kwa jinsi ninavyoona, kifaa hicho kinafanya kazi kama kinavyopaswa. Alipoteza fahamu kwa muda mfupi lakini alirejea haraka na tuliweza kuwasiliana naye mara moja,” amesema Boesen.
Katika mahojiano ya awali kuhusu maisha yake baada ya tukio la Euro 2020, Eriksen aliwahi kueleza namna alivyojifunza kuishi kwa matumaini licha ya changamoto alizopitia.
“Nimejifunza kwamba hata baada ya nyakati ngumu, huwa kuna wakati mwingine ambapo mambo hubadilika. Maisha yana vipindi vya kupanda na kushuka, na muda ndiyo rafiki yako mkubwa,” amesema Eriksen.
Nyota huyo ameendelea kucheza soka la kiwango cha juu tangu alipopona tukio la Euro 2020, na simulizi yake imekuwa chanzo cha hamasa kwa watu wengi duniani wanaopambana na changamoto mbalimbali za kiafya.




