Mastaa

Aunty Ezekiel: Nimezungukwa na nyoka

...ipo siku nitamuweka hadharani

DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini, Aunty Ezekiel, ameibuka na kueleza kuwa amepitia maumivu makubwa kutokana na usaliti wa mtu aliyekuwa akimuamini na kumhesabu kuwa wa karibu.

Kupitia video aliyoweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, Aunty alisema mara nyingi watu huwaita marafiki, ndugu au wasaidizi wao, lakini baadhi yao hugeuka kuwa chanzo cha matatizo makubwa maishani.

Amesema mtu huyo alikuwa akimsaidia hata pale alipokuwa hayupo na alimwamini kwa asilimia kubwa, jambo lililomfanya kumwelezea mara nyingi hadharani kama ndugu, rafiki na mtu wa karibu wa moyo wake.

“Hawa watu ndiyo nyoka, simba na chui. Sijui niwaelezeje, lakini yaliyonikuta Mungu ndiye anayajua.

Nitakuja kuwapa stori kamili kuhusu huyo mtu. Mnajua vizuri tu, nimeshamsifu mara nyingi sana nikimuita ndugu yangu, rafiki yangu na roho yangu,” amesema.

Aunty ameongeza kuwa kwa sasa ameanza kuona ukweli kuhusu tabia ya baadhi ya watu wa karibu, akidai kuna watu wenye mioyo migumu ambao wanaweza kukusababishia matatizo makubwa, hata kufikia hatua ya mtu kwenda gerezani huku akiwaacha watoto wake, wakati aliyemsababishia akiendelea kuishi maisha yake bila kujali.

Kutokana na hali hiyo, msanii huyo amesema amechoka kuvumilia na ameazimia kumweka hadharani mtu huyo ndani ya mwaka huu ili watu wajue kile kilichokuwa kinaendelea.

“Nimeamua mwaka huu nimuweke hadharani watu wajue kinachoendelea, maana nimemvumilia vya kutosha, lakini ameshanifanyia mambo mengi sana,” amesema Aunty Ezekiel.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button