Australia yatawala medali Jumuiya ya madola 2026

SCOTILAND: Mashindano ya Michezo ya Jumuiya ya Madola 2026 (Commonwealth Games) yanayoendelea jijini Glasgow, Scotland, yamezidi kupamba moto huku mataifa mbalimbali yakiongeza idadi ya medali katika siku ya tano ya mashindano.
Kwa mujibu wa jedwali la medali lililosasishwa, Australia imeendelea kuongoza kwa mafanikio makubwa ikiwa na medali 39, zikiwemo 17 za dhahabu, tisa za fedha na 13 za shaba.
England inashika nafasi ya pili kwa jumla ya medali 19, huku wenyeji Scotland wakipanda hadi nafasi ya tatu baada ya kuendelea kufanya vizuri katika michezo mbalimbali.
Mashindano ya leo yamehusisha utoaji wa medali katika michezo ya riadha, kuogelea, mazoezi ya viungo (gymnastics) na kunyanyua uzani, ambapo ushindani umekuwa mkali kati ya mataifa makubwa ya michezo ya Jumuiya ya Madola.
Katika kunyanyua uzani, nyota wa India Mirabai Chanu aliendelea kuandika historia baada ya kutwaa medali ya dhahabu na kuiwezesha nchi yake kuimarisha nafasi kwenye jedwali la medali.
Mashindano ya riadha nayo yameanza kuvutia maelfu ya mashabiki, huku wanariadha wakipambana katika mbio za mchujo na fainali za baadhi ya mataji.
Waogeleaji kutoka Australia na England pia wameendelea kung’ara kwa kutwaa medali muhimu na kuimarisha nafasi za mataifa yao kwenye msimamo wa jumla.
Michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka 2026 imewakutanisha zaidi ya wanamichezo 3,000 kutoka mataifa na maeneo 74, wakishindana katika michezo 10 yenye jumla ya matukio 215 ya kugombea medali.
Mashindano hayo yataendelea hadi Agosti 2, huku mataifa yakisaka kuongeza idadi ya medali na kuwania kumaliza kileleni mwa jedwali la mwisho.




