Kwingineko

Pirlo: Mkataba wangu na kampuni ya Urusi ni wa kibiashara

ROMA: Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Italia, Andrea Pirlo, amevunja ukimya kuhusu mjadala ulioibuka kutokana na ushirikiano wake wa kibiashara na kampuni ya Urusi, huku jina lake likitajwa kuwania nafasi ya kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Italia.

Pirlo alisema aliamua kukaa kimya kwa siku kadhaa kutokana na kuheshimu mchakato unaoendelea ndani ya Shirikisho la Soka Italia pamoja na watu wote wanaohusika.

Katika taarifa yake, Pirlo alisisitiza kuwa maisha yake yote kama mchezaji na kocha amekuwa akiheshimu sheria za nchi alizofanyia kazi pamoja na mikataba aliyosaini.

“Katika kazi yangu yote, kama mchezaji na kocha, nimekuwa nikifanya kazi kwa kufuata sheria za nchi nilizofanyia kazi na mikataba niliyoingia,” alisema Pirlo.

Akizungumzia ushirikiano wake na kampuni hiyo ya Urusi, Pirlo alisema ulianza wakati alipokuwa kocha nchini Falme za Kiarabu (UAE) na ulikuwa na lengo la kibiashara na michezo pekee.

Alikanusha madai kuwa ushirikiano huo unaonesha msimamo wowote wa kisiasa.

Pirlo pia aliwashukuru mastaa wa zamani wa AC Milan, Paolo Maldini na Leonardo, kwa kumuunga mkono na kumuonesha heshima katika kipindi chote cha taaluma yake.

Mshindi wa Kombe la Dunia 2006 na Italia alisema anasikitishwa kuona jambo analoliona kuwa la kibiashara na michezo limegeuka kuwa mjadala mkubwa wa umma.

“Mapenzi yangu kwa Italia ni sehemu ya historia yangu na utambulisho wangu, hayategemei kama nitakuwa kocha wa timu ya taifa au la,” alisema Pirlo.

Related Articles

Back to top button