Azam FC kuwafuata Fountain Gate kwa tahadhari

DAR ES SALAAM: TIMU YA Azam FC imesema inatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa Fountain Gate katika mchezo ujao wa Ligi Kuu baada ya kuonesha kubadilika hivi karibuni chini ya Kocha Fred Minziro.
Akizungumza na Spotileo Ofisa Habari na Mawasiliano wa Azam FC Thabit Zakaria ‘Zakazakazi’ amesema kwa kutambua na umuhimu wa mchezo huo wachezaji wanaendelea kujiandaa vizuri ili kuhakikisha wanakuwa katika hali bora ya ushindani kabla ya kuivaa Fountain Gate.
Zakaria amesema Fountain Gate imekuwa timu tofauti tangu ilipochukuliwa na Kocha Felix Minziro, ambaye ameisaidia kurejea kwenye kiwango kizuri na kupata matokeo chanya katika mechi za hivi karibuni.
“Fountain Gate ni timu ambayo imeamka tena tangu Felix Minziro aichukue. Ni kocha mzuri na ameifanya timu kuwa ngumu kucheza nayo,” amesema.
Ameongeza kuwa timu hiyo imetoka kushinda mabao 2-1 dhidi ya TRA katika mchezo wao uliopita ni ishara ya maendeleo makubwa ya timu hiyo na uwezo wake wa kuleta ushindani mkubwa.
“Wamekuwa wakipata matokeo mazuri wakiwa nyumbani Arusha, hivyo ni lazima tujipange vizuri na kufanya maandalizi ya kutosha ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika mchezo huo,” amesema.



