PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara linafungwa leo kwa michezo minane kupigwa viwanja tofauti kwa wakati mmoja.
Yanga iliyotwaa tayari ubingwa wa 29 wa ligi ipo mkoani Mbeya kufunga pazia na kukabidhiwa kombe itakapoivaa Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Sokoine.
Miamba ya soka nchini Simba itakuwa wenyeji wa Coastal Union kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Polisi Tanzania iliyokwishashuka daraja itakuwa wageni wa Azam inayowania nafasi nne za juu kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Ihefu iliyoanza vibaya ligi lakini baadaye ikazinduka, itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye uwanja wa Highland Estates uliopo Mbarali, Mbeya.
Mechi ya kukata na shoka itakuwa kati ya watoza ushuru wawili, Mbeya City ikiwa mwenyeji KMC kwenye uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga na timu itakayopoteza itakuwa katika hatari ya kucheza mtoani ili kusaka kusalia ligi kuu.
Geita Gold itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Manungu Complex uliopo Turiani, Morogoro.
Kipenzi cha wanasingida, Singida Big Stars imesafiri hadi Lindi kusaka nafasi ya nne bora dhidi ya Namungo kwenye uwanja wa Majaliwa.
Ruvu Shooting baada ya kushuka daraja itamaliza ligi kwa kuikaribisha Dodoma Jiji kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.