Yanga hakuna kulala ni mwendo wa mazoezi

DAR ES SALAAM:KLABU ya Yanga imesema maandalizi ya kikosi chake yanaendelea vizuri kuelekea michezo iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho, huku wachezaji wote wakiwa katika hali nzuri ya afya na utimamu wa mwili.
Akizungumza kuhusu hali ya kikosi hicho, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema benchi la ufundi linaendelea na maandalizi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha timu inafanya vizuri katika mechi zijazo.
Kamwe amesema kwa sasa hakuna mchezaji mwenye majeraha makubwa yanayoweza kuathiri mipango ya timu, jambo ambalo limeongeza morali na ari ya ushindani ndani ya kikosi hicho.
“Maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea mechi za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho. Tunashukuru kwa sasa hakuna majeruhi na wachezaji wote wako tayari kupambana kwa ajili ya kuisaidia Yanga kufikia malengo yake,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa kila mchezaji anatambua umuhimu wa michezo iliyobaki katika msimu huu, hivyo juhudi zinaendelea kuhakikisha timu inabaki katika kiwango bora cha ushindani.
Katika mchezo wake ujao wa Ligi Kuu, Yanga inatarajiwa kusafiri kwenda mkoani Kigoma ambako itavaana na Mashujaa FC Juni 13 katika Uwanja wa Lake Tanganyika.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku Yanga ikilenga kuendelea kukusanya pointi muhimu katika mbio zake za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.




