Hersi:Dhamira yetu ni kubeba makombe yote
RAIS wa Yanga, Injinia Hersi Said amesema dhamira yao ni kuona wanatwaa mataji kwa kila mashindano wanayoshiriki na wanaweza kuwa timu ya kwanza kuleta kombe la Afrika nchini.
Kesho Jumamosi Agosti 17, Yanga itatupa karata yake ya kwanza katika mchezo wa hatua ya awali ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Vital’o ya Burundi, uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi jijini.
Ameongeza kuwa kocha Miguel Gamondi na vijana wake wanakamilisha maandalizi kuelekea mchezo huo na dhamira yao ni kupata ushindi mnono kujihakikishia kutinga raundi ya kwanza ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa.
“Dhamira yetu kila mashindano tunayoshiriki tunataka kubeba kombe, katika mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa, tukiweka dhamira kubwa na kwa baraka za Mungu kwanini tusiwe timu ya kwanza kuleta kombe la Afrika hapa Tanzania?,” amesema Hersi.
Kuhusu usajili wa kiungo Clatous Chama amesema haikuwa rahisi kumsajili kiungo wao mshambuliaji huyo kwani ni moja ya wachezaji bora zaidi waliowahi kutokea katika ligi kuu Tanzania Bara na nafasi yake ni kubwa sana kwenye timu.
“Mmoja kati ya wachezaji waliowahi kucheza kwenye ligi kuu niliokuwa navutiwa nao hapa nchini, ni Chama. Ni mmoja kati ya wachezaji bora na kwa kiwango alichokuwa nacho, atakuwa na mchango mkubwa sana”, amesema Hersi.