Opa: Ushirikiano ndiyo siri ya ushindi wa Twiga Stars

DAR ES SALAAM:NAHODHA wa Timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania, Twiga Stars, Opa Clement, amesema ushirikiano mkubwa miongoni mwa wachezaji ndio uliowezesha timu hiyo kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Malawi katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Twiga Stars iliibuka na ushindi huo kupitia bao pekee lililofungwa na Opa Clement, ambaye pia aliongoza timu hiyo katika mchezo huo.
Akizungumza baada ya mechi, Opa alimshukuru Mungu kwa ushindi huo na kuwapongeza wachezaji wenzake kwa kujituma na kushirikiana kwa kiwango kikubwa uwanjani.
“Kilichotupa ushindi ni ushirikiano kati yangu na wachezaji wenzangu. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa matokeo haya na sasa tunajipanga kwa ajili ya mechi inayofuata,” amesema Opa.
Hata hivyo, nahodha huyo alibainisha kuwa timu haikuwa na muda wa kutosha wa maandalizi kabla ya mchezo huo, jambo ambalo lilikuwa changamoto kwa kikosi hicho.
Licha ya hali hiyo, Opa anaamini Twiga Stars itaonesha kiwango bora zaidi katika mchezo wa pili kutokana na kupata nafasi ya kufanya mazoezi pamoja na kuimarisha mshikamano ndani ya kikosi.
“Naamini kabla ya mechi ya pili tutapata muda wa kufanya mazoezi kwa pamoja. Nawaahidi Watanzania tutafanya vizuri zaidi katika mchezo unaofuata,” amesema.
Aidha, amewahimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo na kuendelea kuiombea ili iweze kupata matokeo mazuri katika michezo yake ijayo.




