Kwingineko

Timu ya Taifa ya Kenya yakwama Hotelini Afrika Kusini

PRETORIA: KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Stars) kimejikuta kwenye sintofahamu nchini Afrika Kusini baada ya kukwama hotelini kutokana na mgogoro wa malazi na malipo wakati kikijiandaa na mechi mbili za kirafiki dhidi ya Lesotho.

Taarifa zinaeleza kuwa mara baada ya kuwasili Pretoria, baadhi ya wachezaji walikataa kuingia katika hoteli ya kwanza waliyoandaliwa wakidai kuwa haikukidhi hadhi na viwango vinavyostahili kwa timu ya taifa.

Baada ya malalamiko hayo, viongozi wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) walifanikiwa kutafuta hoteli nyingine na kuhamishia kikosi huko. Hata hivyo, changamoto mpya ilizuka baada ya uongozi wa hoteli hiyo kudai malipo ya haraka kabla ya kuruhusu wageni kuingia vyumbani.

Kutokana na kutokubaliana kuhusu utaratibu wa malipo, wachezaji na viongozi walilazimika kusubiri kwa saa kadhaa katika eneo la mapokezi huku wakisubiri suluhu ya mgogoro huo.

Baadaye usiku taarifa zilieleza kuwa tatizo hilo lilitatuliwa na wachezaji wakaruhusiwa kuingia vyumbani mwao tayari kwa maandalizi ya michezo hiyo ya kirafiki.

Tukio hilo limezua mjadala mkubwa mitandaoni, huku mashabiki wengi wakihoji namna maandalizi ya safari za timu ya taifa yanavyosimamiwa.

Harambee Stars ipo nchini Afrika Kusini kwa ajili ya mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya Lesotho ikiwa sehemu ya maandalizi ya majukumu yajayo, ikiwemo kampeni za kufuzu AFCON 2027.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button