Ruben Dias:Ureno tunataka ubingwa wa Dunia

LISBON:BEKI wa kimataifa wa Ureno, Ruben Dias , amesema kikosi cha taifa lake kinaingia kwenye mashindano ya Kombe la Dunia 2026 kikiwa na unyenyekevu lakini pia kikiwa na azma kubwa kuliko wakati wowote uliopita wa kuhakikisha wanachukua ubingwa.
Akizungumza kuelekea mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Dias amesema hii itakuwa Kombe la Dunia lake la tatu na anaona ni nafasi maalum kwa wachezaji, mashabiki na taifa la Ureno kwa ujumla.
Dias amesema kuwa Ureno imeendelea kunufaika na umoja wa kikosi chao, ambapo mahusiano mazuri kati ya wachezaji yamekuwa chachu ya mafanikio ndani na nje ya uwanja.
Pia, amemzungumzia nahodha wa Ureno Christiano Ronaldo, akisema amejifunza mengi kutoka kwake pamoja na wachezaji wengine wenye uzoefu kama Pepe, ambao wamekuwa chanzo kikubwa cha uongozi na hamasa.
Ureno imepangwa kucheza hatua ya makundi dhidi ya DR Congo, Uzbekistan na Colombia katika Kundi K, michezo itakayofanyika Marekani.
Licha ya kutajwa kuwa miongoni mwa timu zinazoweza kufanya vizuri, Dias amesema Ureno inabaki na unyenyekevu lakini ina azma kubwa ya kufanya historia kwa kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.



