Gor Mahia waingiza zaidi ya milioni 110 siku ya Ubingwa Na Festo Polea

NAIROBI: MASHABIKI wa Mabingwa wa soka la Kenya 2025/26 Gor Mahia wameinufaisha timu yao iliingiza Nyayo kuwa bahari ya kijani na nyeupe huku klabu hiyo ikikusanya zaidi ya milioni 5.45 ambazo ni zaidi ya milioni 110 kupitia mauzo ya tiketi katika mechi ya kutawazwa mabingwa wa msimu wa 2025/26 wa SportPesa Premier League.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mtunza hazina wa klabu hiyo, Gerphas Okuku, jumla ya tiketi 17,487 ziliuzwa katika mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Nairobi United FC.
Ingawa Gor Mahia walipoteza mechi hiyo, hilo halikupunguza shamrashamra za mashabiki wake waliokuwa wamejitokeza kusherehekea ubingwa wa kihistoria wa 22 wa ligi ya Kenya.
Maelfu ya mashabiki walijaza Uwanja wa Nyayo kushuhudia wachezaji, viongozi wa klabu na magwiji wa zamani wakisherehekea mafanikio hayo makubwa.
Klabu hiyo pia iliipongeza kampuni ya LangoPass kwa mchango wake katika mfumo wa tiketi za kidijitali uliosaidia kuongeza uwazi na ukusanyaji wa mapato.
Taarifa za mapato hayo zilichochea mjadala mkubwa mtandaoni, huku wengi wakisifia mwamko mpya wa soka la Kenya. Baadhi ya mashabiki walieleza kuwa mafanikio hayo yanaonesha nguvu kubwa ya mashabiki wa Gor Mahia na uwezo wa soka la Kenya kujitegemea kifedha.
Mapato hayo yanatajwa kuwa kichocheo kikubwa kwa klabu hiyo kuelekea msimu mpya pamoja na mashindano ya kimataifa yanayoisubiri.




