Kwingineko

Mmiliki wa Southampton amkingia kifua Kocha Mkuu

SOUTHAMPTON: MMILIKI wa klabu ya Southampton nchini England Dragan Solak, amesema hatamfukuza kazi kocha mkuu wa timu hiyo Tonda Eckert, licha ya kuhusishwa na sakata la kupeleleza mazoezi ya timu pinzani katika Championship.

Solak amesema Eckert anastahili kupewa nafasi ya pili kutokana na uwezo wake mkubwa wa ukocha na mchango alioutoa tangu alipopewa jukumu la kuiongoza Southampton mwezi Desemba mwaka jana.

“Nadhani anastahili nafasi ya pili na niko tayari kumpa. Anaungwa mkono kikamilifu kwa sababu ni kocha mwenye kipaji kikubwa,” amesmea Solak katika mahojiano maalumu na BBC.

Eckert aliiokoa Southampton kutoka katika hatari ya kushuka daraja na kuifikisha timu hiyo hadi hatua za mtoano za kuwania kupanda Ligi Kuu England baada ya kumaliza katika nafasi ya nne. Hata hivyo, klabu hiyo iliondolewa kwenye hatua hizo baada ya kukiri kufuatilia mazoezi ya wapinzani wake, jambo lililosababisha kupewa adhabu ya kuanza msimu wa 2026/27 ikiwa imekatwa pointi nne.

Tume huru ya nidhamu ilibaini kuwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 33 alihusika katika kupanga mpango wa kufuatilia mazoezi ya timu pinzani, huku Southampton ikikiri makosa hayo dhidi ya Oxford United, Ipswich Town na Middlesbrough.

Licha ya sakata hilo, Solak amesema anaamini Eckert hakujua kuwa kitendo hicho kilikiuka kanuni za English Football League (EFL), akisisitiza kuwa bodi ya klabu inaendelea kumuamini.

Hata hivyo, Solak amesema amempa onyo kali kocha huyo na kumtaka kuhakikisha anazifahamu kikamilifu kanuni za EFL ili kuepusha matatizo kama hayo siku zijazo.

Mmiliki huyo pia amepinga ukubwa wa adhabu waliyopewa, akidai kuwa imekuwa kubwa kuliko kosa lenyewe na imeigharimu klabu nafasi ya kuwania mapato makubwa yaliyoweza kupatikana iwapo wangefanikiwa kupanda Ligi Kuu.

Wakati huo huo, Chama cha Soka England (FA) kinaendelea kuchunguza sakata hilo na kinaweza kuchukua hatua zaidi dhidi ya Eckert. Solak amesema ataendelea kumuunga mkono kocha huyo hata kama atakumbana na adhabu nyingine kutoka kwa mamlaka za soka nchini humo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button