Kwingineko

Mendy: Kukosa umakini kuliigharimu Senegal dhidi ya Ufaransa

EAST RUTHERFORD, Marekani: Kipa wa timu ya taifa ya Senegal, Edouard Mendy, amesema kukosa umakini katika nyakati muhimu za mchezo ndiko kulikochangia timu yake kupoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Ufaransa katika mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia uliochezwa Jumanne.

Senegal ilianza mchezo huo kwa kiwango kizuri na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga katika kipindi cha kwanza, lakini ilishindwa kuzitumia ipasavyo. Ufaransa ilitumia makosa hayo na kuibuka na ushindi kupitia mabao mawili ya Kylian Mbappe na moja la Bradley Barcola.

Bao pekee la Senegal lilifungwa na Ibrahim Mbaye, lakini halikutosha kuzuia kipigo hicho dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa dunia.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mendy alisema wachezaji wa Senegal walishindwa kutekeleza mpango wao wa mchezo licha ya kuwa na mwanzo mzuri.

“Tulikuwa wazito kidogo katika kipindi cha kwanza. Tulijua kwamba katika kipindi cha pili tulipaswa kuongeza kasi na kuwa makali zaidi katika eneo la ushambuliaji,” alisema Mendy.

Kipa huyo mwenye umri wa miaka 34 aliongeza kuwa dhidi ya timu yenye ubora mkubwa kama Ufaransa, makosa madogo yanaweza kugharimu matokeo ya mchezo.

“Dhidi ya timu kama hizi unapaswa kuwa makini kwa asilimia mia moja katika ushambuliaji na ulinzi. Huwezi kupoteza umakini hata kwa sekunde chache kwa sababu unakutana na wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu,” alisema.

Mendy, ambaye aliwahi kushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea mwaka 2021, alisisitiza kuwa tofauti kati ya Senegal na Ufaransa si kubwa kama ambavyo matokeo yanaweza kuonesha.
Senegal, iliyowahi kufika robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2002, inatarajiwa kucheza dhidi ya Norway Jumatatu ijayo kabla ya kuhitimisha mechi za makundi kwa kuikabili Iraq siku nne baadaye.

“Nilisema hata kama tungeushinda mchezo huu, kundi bado lingekuwa wazi. Tumepoteza leo, lakini kama ilivyokuwa mwaka 2022, tunapaswa kujipanga upya, kupumzika na kuelekeza nguvu zote kwenye mchezo dhidi ya Norway,” alisema Mendy.

Related Articles

Back to top button