Serena kurudi uwanjani baada ya miaka minne

LONDON: NYOTA wa zamani wa tenisi duniani, Serena Williams, anatarajiwa kurejea tena kwenye mashindano ya ushindani baada ya taarifa kueleza kuwa huenda akacheza michuano ya Queen’s Club mwezi ujao nchini England.
Serena mwenye umri wa miaka 44 hajacheza mchezo wa ushindani tangu mwaka 2022 alipostaafu baada ya michuano ya US Open, lakini sasa ameibua matumaini ya kurejea uwanjani katika mashindano ya WTA 500 yatakayofanyika jijini London.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, bingwa huyo wa mataji 23 ya Grand Slam anatarajiwa kucheza mashindano ya watu wawili (doubles) ikiwa atapatiwa nafasi maalum ya wildcard.
Mashindano hayo yataanza Juni 8 huku Wimbledon ikitarajiwa kuanza wiki tatu baadaye, jambo linalozidi kuongeza uvumi kuhusu uwezekano wa Serena kurejea rasmi kwenye mashindano makubwa.
Taarifa zinaeleza kuwa Serena amekamilisha masharti ya kurejea kwenye mfumo wa vipimo vya dawa za michezo na sasa yupo huru kushiriki tena mashindano ya kitaalamu.
Nyota huyo ambaye aliwahi kutwaa mataji saba ya Wimbledon katika mchezo wa mmoja mmoja pamoja na mataji saba ya doubles akiwa na dada yake Venus Williams, anaendelea kutajwa kama mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya tenisi.
Ingawa hakuna uthibitisho rasmi kuhusu mshirika wake wa doubles, taarifa mbalimbali zimehusisha jina lake na mchezaji chipukizi kutoka Canada, Victoria Mboko mwenye miaka 19.
Katika miaka ya hivi karibuni Serena amekuwa akizungumzia safari yake ya kurejea katika utimamu wa mwili baada ya kupunguza uzito huku akiendelea kufanya mazoezi makali.
Iwapo atarejea rasmi uwanjani, hatua hiyo itakuwa moja ya habari kubwa zaidi katika ulimwengu wa tenisi kutokana na historia na mafanikio makubwa aliyoyapata ndani ya mchezo huo.




