Ligi Kuu

TRA tumewazidi kila kitu- Bwire

ARUSHA: JKT Tanzania imesema haiwezi kujifananisha  na TRA United kwani wameizidi ubora, malengo na uimara wa kikosi.

Akizungumza baada ya mchezo jana Ofisa Habari wa JKT Tanzania, Masau Bwire amesema mashabiki waliofuatilia mchezo huo wamejionea tofauti ya viwango kati ya timu hizo mbili huku akisisitiza kuwa wapinzani wao walinusurika kupata matokeo mabaya zaidi.

“JKT Tanzania huwezi kuilinganisha na timu kama TRA, tumewaacha kwa kila kitu, ubora wa timu na malengo. Wao bado wanajitafuta,” amesema.

Amedai kuwa wachezaji waliokuwa wakipewa sifa kubwa kabla ya mchezo huo walishindwa kuonesha ubora mbele ya kikosi cha JKT Tanzania.

“Watanzania waliofuatilia mpira wameona nini kimetokea. Walikuwa wanasikia Chobwedo lakini leo wamegeuka kuwa Domwechi. Hakuna kitu anachokifanya mbele ya waliobora. Hiyo ndiyo JKT Tanzania,” amesema.

Aidha, amesema baadhi ya timu zilizowahi kupata matokeo mazuri dhidi yao zilijenga taswira tofauti kuhusu uwezo wa JKT Tanzania, lakini mchezo huo umeonesha kiwango halisi cha timu hiyo.

“Kuna timu kadhaa zilipita hapa wakapata matokeo mazuri wakadhani JKT iko hivyo, wameponea tundu la sindano. Hakika wameona sisi sio kiwango chao,” amesema.

Bwire ameongeza kuwa JKT Tanzania haitumii maneno ya mipasho bali inaamini katika kuonesha uwezo ndani ya uwanja.

Related Articles

Back to top button