Burudani

Washiriki 20 BSS watinga kambini

DAR ES SALAAM: WASHIRIKI 20 kutoka Kenya, Uganda, DR Congo na Tanzania waliochaguliwa kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania pamoja na nchi kadhaa za Afrika Mashariki na Kati wamewasili rasmi kambini katika ufukwe wa Ndege Beach jijini Dar es Salaam kuanza safari yao ya kutwaa ushindi vipaji la Bongo Star Search (BSS).

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Azam Media jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Benchmark Production na muandaaji wa shindano hilo, Rita Paulsen, amesema msimu wa mwaka huu umebeba ushindani mkubwa zaidi kutokana na kiwango cha juu cha vipaji vilivyojitokeza wakati wa usaili.

Rita amesema kundi hilo linajumuisha washiriki 10 wa Tanzania, watatu wa Kenya, wawili wa Uganda, watatu wa DR Congo pamoja na kundi moja la wachezaji wa dansi na mchekeshaji mmoja kutoka Mbeya.

“Washiriki wa mwaka huu wana viwango vya juu sana. Kuna tofauti kubwa ukilinganisha na misimu iliyopita, jambo linaloonesha ukuaji wa sekta ya burudani,” amesema Rita.

Ameeleza kuwa hatua ya kwanza kambini itahusisha utambulisho wa washiriki, ambapo kila mmoja atajieleza, kueleza historia yake pamoja na safari yake ya kipaji chake.

Rita ameongeza kuwa majaji walipata wakati mgumu kuchagua washiriki wa mwisho kutokana na ushindani mkubwa uliojitokeza wakati wa usaili.

Kuhusu uwepo wa mchekeshaji mmoja pekee, Rita amefafanua kuwa licha ya wengi kujitokeza, wengi wao hawakufikia viwango vya kitaalamu vilivyohitajika katika kipengele cha uchekeshaji ndani ya mashindano hayo.

“Haya ni mashindano. Hakuna upendeleo. Kila mmoja ana nafasi sawa ya kuonesha kipaji chake. Uchekeshaji ni kipaji kinachohitaji ubunifu mkubwa na mwendelezo ukilinganisha na vipaji vingine kama uimbaji,” ameongeza.

Shindano hilo linalorushwa na Azam TV kupitia chaneli ya Sinema Zetu litaendelea kwa hatua mbalimbali za mchujo hadi kupatikana mshindi wa mwisho katika fainali kuu.

Related Articles

Back to top button