World Cup

DSTV yazindua ‘kila kitu kitasubiri’ kuelekea Kombe la Dunia

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya DStv kupitia SuperSport imezindua kampeni yake mpya ya “Kila Kitu Kitasubiri” kuelekea fainali za Kombe la Dunia 2026 huku ikitangaza maboresho makubwa ya huduma kwa mashabiki wa soka nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Masoko wa DStv, Ronald Shelukindo amesema Kombe la Dunia linaendelea kuwa mashindano makubwa zaidi duniani kutokana na idadi kubwa ya watazamaji wanaofuatilia michuano hiyo.

Shelukindo amesema katika fainali za mwaka 2022 zaidi ya watu bilioni tano walifuatilia mashindano hayo, jambo linalothibitisha ukubwa wake duniani.

Amesema fainali zijazo zinatarajiwa kuvunja rekodi zaidi kutokana na ongezeko la timu kutoka 32 hadi 48 pamoja na idadi ya mechi kuongezeka kutoka 68 hadi 104.

“Kwa upande wa Afrika tutakuwa na uwakilishi wa timu 10 hivyo tunatarajia ushindani mkubwa zaidi na hamasa kubwa kwa mashabiki wa soka barani Afrika,” amesema Shelukindo.

Mashindano hayo yatafanyika kwa mara ya kwanza katika mataifa matatu ambayo ni Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 2026.

Katika maboresho hayo, DStv imetangaza kuwa kwa kipindi chote cha mashindano, chaneli ya SuperSport EPLA namba 223 itabadilishwa jina na kuwa SuperSport FIFA World Cup 2026 ambayo itarusha mechi zote hadi kwenye kifurushi cha Bomba.

Shelukindo amesema hiyo ni sehemu ya kuhakikisha mashabiki wengi zaidi wanapata nafasi ya kushuhudia michuano hiyo mikubwa kwa gharama nafuu.

“Kwa mara ya kwanza mechi za Kombe la Dunia zitaoneshwa hadi kwenye kifurushi cha Bomba” amesema.

Aidha, amesema wateja wenye dish tayari watanunua dikoda kwa Sh15,000 huku wanaohitaji kifurushi kamili pamoja na dish wakitakiwa kulipa Sh45,000.

Pia amesema kutakuwa na chaneli maalum kwa Tanzania itakayorusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili ili kuwapa urahisi zaidi watazamaji wa ndani kufuatilia mashindano hayo.

Mbali na hayo, Shelukindo alieleza baadhi ya historia za kipekee za Kombe la Dunia ikiwemo tukio la kombe hilo kuibwa na baadaye kupatikana kwa msaada wa mbwa, huku tukio jingine la wizi likitokea mwaka 1983 nchini Brazil.

 

Related Articles

Back to top button