Parker aondoka Burnley baada ya kushuka daraja

LONDON:KOCHA Mkuu wa Burnley, Scott Parker, ameondoka klabuni hapo kwa makubaliano ya pande zote, siku nane tu baada ya timu hiyo kuthibitisha kushuka daraja kutoka Premier League.
Hatua hiyo inakuja kufuatia msimu mgumu kwa Burnley, ambao umeshuhudia timu hiyo ikishinda michezo minne pekee kati ya 34 ya ligi, huku ikikusanya pointi moja tu katika michezo yake minane ya mwisho.
Katika taarifa yake, Parker amesema kuinoa Burnley ilikuwa heshima kubwa kwake, lakini wakati umefika kwa kila upande kuchukua mwelekeo mpya.
“Ilikuwa heshima kubwa kuiongoza klabu hii kwa miaka miwili iliyopita. Nimefurahia kila hatua ya safari yetu, lakini ninaamini huu ndio wakati sahihi kwa kila upande kwenda njia tofauti,” amesema Parker.
Kocha huyo pia alikumbushia mafanikio yao ya msimu wa 2024-25, alipoiwezesha Burnley kupanda daraja kurejea Ligi Kuu, jambo alilolitaja kuwa ni fahari kubwa kwake.
“Ninajivunia tulichokifanya, hasa msimu wa kupanda daraja ambao hautasahaulika. Ilikuwa heshima kuiongoza timu hii katika Premier League,” ameongeza.
Kwa sasa, msaidizi wake, Mike Jackson, atachukua jukumu la muda kuinoa timu hiyo katika michezo minne iliyosalia ya msimu, wakianza na mchezo dhidi ya Leeds United.
Mbali na matokeo mabaya ya ligi, Burnley pia ilipata misukosuko kwenye michuano ya vikombe, ikitolewa mapema katika FA Cup na Carabao Cup na timu za daraja la chini, hali iliyochangia uamuzi huo wa mabadiliko ya benchi la ufundi.
Kuondoka kwa Parker kunafungua ukurasa mpya kwa Burnley, ambayo sasa italazimika kujipanga upya kwa ajili ya maisha ya Championship msimu ujao.




