Slot ahofia majeraha ya Ekitike

LONDON, England: Kocha wa Liverpool FC, Arne Slot, amesema ana hofu kubwa kuhusu hali ya mshambuliaji Hugo Ekitike kufuatia kupata jeraha baya katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain.
Ekitike alitolewa nje kwa machela dakika ya 30 ya mchezo wa robo fainali mkondo wa pili baada ya kuanguka bila kuguswa na mchezaji yeyote.
Nyota huyo wa Ufaransa alionekana kushika kifundo cha mguu huku akionesha maumivu makali kabla ya kuondolewa uwanjani.
Liverpool ilipoteza mchezo huo kwa mabao 2-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-0 dhidi ya PSG.
Akizungumza baada ya mechi, Slot amesema hali ya mchezaji huyo inaonekana si nzuri:
“Ekitike anaonekana kuwa katika hali mbaya, lakini ni vigumu kusema ni kwa kiwango gani. Haionekani vizuri, hilo liko wazi,” amesema.

Ekitike, ambaye yupo katika msimu wake wa kwanza Anfield baada ya kujiunga kutoka Eintracht Frankfurt, tayari amefunga mabao 17 katika mechi 45 msimu huu, yakiwemo 11 katika Ligi Kuu England.
Jeraha hilo linaweza kuwa pigo kubwa kwake binafsi, hasa wakati huu ambapo anatarajia kuwania nafasi katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kuelekea Kombe la Dunia la majira ya kiangazi.
Beki wa Liverpool na timu ya taifa ya Ufaransa, Ibrahima Konate, amesema tukio hilo ni pigo kubwa kwa mchezaji mwenzake.
“Nadhani ni jeraha baya. Ni wakati mgumu sana kwake hasa ukizingatia Kombe la Dunia linakuja,” amesema Konate.
Sasa mashabiki wa Liverpool wanasubiri majibu rasmi ya vipimo vya kitabibu ili kujua ukubwa wa jeraha hilo na muda ambao Ekitike atakaa nje ya uwanja.




