Armee Sebene: Bendi ya wanaume tupu inayotikisa Morogoro
MOROGORO: MJI wa Morogoro umeendelea kujizolea umaarufu mkubwa kwa kutoa vipaji kwenye tasnia ya muziki na hakika wasanii hao wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa tangu enzi za kina Mbaraka Mwishehe mpaka leo hii.
Armed Sebene ni moja ya bendi maarufu zinazokuja kwa kasi kutoka Morogoro ikiwa imejikita zaidi katika muziki wa gospo na tayari wamefanikiwa kuwa na maelfu ya mashabiki ndani na nje ya mji huo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita bendi hiyo ilifanikiwa kufanya onyesho lake kubwa katika ukumbi wa Sapna Hall Barabara ya Stesheni Manispaa na kuendelea kuweka rekodi ya kipekee katika muziki huo wa live.
Akizungumza na Spotileo siku chache baada ya onyesho hilo kiongozi wa bendi hiyo Shetente Meshack amesema Usiku huo uliopewa jina la The Weekend na Armee Sebene chini ya kanisa la Global Church For All Nations, umeweka alama mpya kwao.
“Tumezoea kufanya huduma hizi kikawaida lakini usiku wa leo umekuwa tofauti na tumewabariki wengi kwa nyimbo zetu, huduma hii ya The Weekend na Armee Sebene itakuwa endelevu ndani na nje ya Morogoro,” amesema Shetente.
Akizungumzia lengo ya tukio hilo Mwananzambe amesema: “Huduma hii inalenga kutoa fursa kwa jamii kupata elimu, burudani na matumaini kupitia muziki wa Injili. Armee Sebene inalenga kubadilisha mtazamo wa watu kuelekea maisha chanya na kuchangia katika maendeleo ya jamii, dini na Taifa kwa ujumla.”
Aidha katika jambo la kushangaza la bendi hiyo maarufu kwa muziki aina ya sebene, hawana mwimbaji na mwanamuziki wa kike, wote ni wanaume na hakuna kinachoharibika.
Akizungumzia namna wanavyoweza kufanya kazi wakiwa wanaume peke yake, Mwananzambe, amesema hayo ni maono waliyopewa na Mungu na jukumu lao ni kuyasimamia na kuhakikisha yanafanikiwa.
” Sisi hatuna mwimbaji wa kike wala mwanamuziki wa kike, kuanzia sauti ya kwanza mpaka ya tatu tunaimba sisi wenyewe na katika hilo tumemuona Mungu na watu wanaguswa na huduma yetu kama Armee Sebene katika kuleta mabadiliko chanya,” amesema Shetente.
Aliongeza kuwa Armee Sebene ni bendi iliyojikita katika muziki wa sebene kwasababu ni muzikin unaopendwa na wengi na kupitia aina hiyo ya muziki wataweza kuokoa nafsi za vijana wengi ambao huufuata muziki huo kwenye baa na matamasha ya muziki wa dansi.
“Sebene ni muziki mzuri unaopendwa na vijana wengi wanaufata huko kwenye baa na sehemu za starehe lakini sisi tunaufanya ili hao vijana wampende Mungu na tumeshaanza kufanikiwa kwenye hilo,” amesema kiongozi wa Armee Sebene, Shetente Meshack