Mpira wa Wavu wapata msukumo kukuza vipaji

DAR ES SALAAM: MPIRA wa wavu nchini umepata msukumo mpya wa kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana baada ya kampuni ya mawasiliano ya Yas kuingia ushirikiano na Chama cha Mpira wa Wavu nchini.
Ushirikiano huo unalenga kuinua kiwango cha mchezo huo kupitia udhamini unaolenga kutoa motisha kwa wachezaji pamoja na waamuzi, sambamba na kuhamasisha ushiriki mpana wa vijana katika mchezo huo.
Akizungumza wakati wa utambulisho wa udhamini huo, Meneja Biashara wa Yas, Divine Amani Mosi, amesema lengo la ushirikiano huo ni kuhakikisha mchezo wa mpira wa wavu unaendelea kukua huku ukibeba jukumu la kukuza vipaji na kuleta fursa kwa vijana.
Amesema katika hatua ya awali, kampuni hiyo itatoa medali 250 kwa wachezaji zitakazotolewa mwishoni mwa ligi, pamoja na mahema ya kujikinga na mvua na jua. Aidha, kutakuwa na zawadi mbalimbali ikiwemo bando la mwezi kwa mchezaji bora wa kiume na kike pamoja na mwamuzi bora wa kila wiki.
“Tunafanya mazungumzo na viongozi wa chama ili kuboresha zaidi ushirikiano huu. Mambo yatakapokamilika tutatoa taarifa rasmi,” amesema.
Katika hatua nyingine, wachezaji waliofanya vizuri ligi ya mkoa wa Dar es Salaam wamepewa tuzo. Wachezaji hao ni Evance Masinga kutoka klabu ya Best Six, aliyesema tuzo aliyopata ni matokeo ya juhudi na kujituma uwanjani.
Naye mchezaji bora wa kike kutoka Bandari, Sara Hengama, amesema siri ya mafanikio yake ni kujituma katika mazoezi binafsi sambamba na yale ya timu, akiwahimiza wachezaji wengine kufanya vivyo hivyo.



