Simba hakuna kukata tamaa!

ARUSHA: MENEJA Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema sare ya bila kufungana dhidi ya TRA haijaathiri malengo ya timu hiyo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Ahmed amekiri kuwa matokeo hayo hayakuwa ya kuridhisha lakini hayajapunguza ari ya kikosi hicho kupambana hadi mwisho wa msimu.
“Bado mbio za ubingwa ziko wazi. Sare dhidi ya TRA haijatukatisha tamaa wala kutuondoa katika mipango yetu, tunaendelea kupambana,” amesema.
Ameeleza kuwa mchezo dhidi ya TRA ulikuwa mgumu kama ilivyo kwa timu nyingine zote zinazowania ubingwa, akibainisha kuwa matokeo kama hayo ni sehemu ya ushindani wa ligi.
“Tunafahamu mechi ya TRA ni ngumu, na kwa wanaowania ubingwa lazima wakutane na matokeo ya aina hii,” aliongeza.
Ahmed aliwataka mashabiki wa Simba kuendelea kuwa na imani na timu yao licha ya matokeo hayo na kuelekeza nguvu kubwa kwenye mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Dodoma Jiji, akieleza kuwa ni mechi ya mtoano inayohitaji umakini mkubwa.
“Ni mechi ngumu ya mtoano, ukipoteza unaondolewa. Tunaamini tuna nafasi kubwa ya kufanya vizuri na kuchukua ubingwa,” amesema.




