Ligi KuuNyumbani

LIGI KUU TANZANIA BARA: Simba, Yanga, Azam ni hatari zaidi

USIOMBE ukutane na timu hizi bora Tanzania unaweza kusema hivyo, kutokana na kasi zao walizoanza nazo msimu huu katika mechi za awali za Ligi Kuu Soka Tanzania Bara.

Ubora wake unatokana na usajili wa kila mmoja na hatari walizoonesha katika mechi mbili ambazo kila mmoja amecheza na kushinda zote wakitoa tahadhari kwa wapinzani,
wakitambiana na kujiona wao ni zaidi ya wengine.

YANGA AFRICANS
Hawa ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mpaka sasa wameonesha
utayari wa kutetea tena ubingwa wao kwa msimu watatu mfululizo na ni tofauti kabisa na matarajio ya wengi.

Ilidhaniwa kuwa kuondoka kwa baadhi ya wachezaji na kuvunjika kwa benchi la ufundi
kutawapa wakati mgumu kujitengeneza na kurudi na kasi yao ya misimu miwili iliyopita
lakini wameonesha kitu tofauti.

Aliondoka mshambuliaji wao hatari Fiston Mayele aliyejiunga na Pyramids ya Misri, Yanick Bangala na Feisal Salum waliojiunga na Azam FC, Djuma Shabani na wengine wametemwa kutokana na kushindwa kuendana na kasi mpya.

Wakasajili wachezaji wasiokuwa na majina makubwa kama Max Nzengeli kutoka AS Maniema ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Pacome Zouzoua na Yao Attouhoula kutoka Asec Mimosas, Hafiz Konkoni kutoka Ghana, Gift Fred kutoka Uganda na wengine.

Karibu wachezaji saba wapya chini ya benchi la ufundi jipya linaloongozwa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi. Timu hii imewashangaza watu katika michezo ya mashindano mitano waliyocheza wamefunga mabao mengi wakiruhusu bao moja tu kwenye nyavu zao.

Katika mechi za Ngao ya Jamii walifunga mabao 2-0 dhidi ya Azam FC, mabao 7-1 dhidi ya Asas ya Djibouti mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, wa kwanza 2-0 na wa pili 5-1 kisha kwenye ligi wakaifunga KMC mabao 5-0 na 5-0 dhidi ya JKT Tanzania.

Wamefunga jumla ya mabao 19 kuonesha namna walivyo hatari na wanapaswa kuogopwa na wapinzani. Chini ya mfumo wa Gamondi, Yanga imekuwa ikicheza kwa kasi, pasi, soka la kuvutia na kila mchezaji anaweza kufunga kwa sasa hawategemei mshambuliaji pekee ndio afunge.

Anaweza kufunga yeyote anayepata nafasi ikiwa ni beki, kiungo, winga au mshambuliaji.
Yanga katika michezo miwili ya ligi imefunga mabao 10 na kupanda hadi kwenye uongozi wa ligi kwa tofauti ya mabao mengi ya kufunga lakini pia haijaguswa nyavu zake.

Hilo lina faida kwao ndio imewasaidia kupata ushindi mkubwa na kama wataendelea hivyo, katika mechi zijazo basi wapinzani wajiandae mapema wakijua Yanga sio wa kubezwa bali kujipanga namna ya kuwadhibiti wasiingie katika ngome zao kiurahisi.

AZAM FC
Timu ya pili kwa utayari ni Azam FC. Lakini timu hii imekuwa na mazoea ya kuanza kwa kasi Ligi Kuu Bara na kumaliza katika nafasi ya tatu au nne, lakini msimu huu labda inaweza kubadilika licha ya kuendelea kutolewa mapema katika michuano ya kimataifa.

Azam imetolewa katika raundi ya awali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Katika michezo miwili ya Ligi Kuu wamefunga mabao saba wakishika nafasi ya pili kwa pointi sawa na Yanga pamoja na Simba kila moja ikiwa na pointi sita.

Waliichapa timu ngumu Tanzania Prisons mabao 3-1 kisha baadaye wakaichapa Tabora
United mabao 4-0. Ushindi huo unaonesha wazi hawapaswi kubezwa na wakiendelea hivyo hadi mwisho basi taji la ubingwa litakuwa kazi kutabiri.

Wameruhusu bao moja kwenye nyavu zake. Bado safu yao ya ulinzi inapewa mashaka. Ukiacha kwenye ligi. Katika michuano ya kimataifa walifungana mabao 2-1 kwenye michezo miwili. Wakatolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Katika michuano ya Ngao ya Jamii walifungwa mabao 2-0 dhidi ya Yanga na wao wakaifunga Singida Big Stars mabao 2-0 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.

Azam FC sio wabovu na wala hawapaswi kubezwa kwa sababu baada ya kutolewa michuano ya Kombe la Shirikisho na timu ya Ethiopia ya Bahir Dar watu waliwazonga na kuwarushia maneno ya hapa na pale.

Kuna fikra zimejengeka kwamba huwa wanaanza na kasi kisha mwisho wao mbaya huanza kuboronga. Sasa wanapaswa kujitathmini na kuondoa yale mazoea kwa kuhakikisha wanafanya vizuri na kuendelea kuleta ushindani mpaka mwisho wa ligi.

Kwa takwimu zake, ni timu hatari inayopaswa kuchungwa na atakayeichukulia kimazoea anaweza kuumbuka.

SIMBA SPORTS
Kwa upande wa Simba nayo ni hatari tupu. Usajili wao msimu huu walionesha wazi wanataka kurejesha kasi yao ya kuchukua mataji baada ya kuyakosa misimu miwili mfululizo.

Wamefanya usajili mkubwa wa wachezaji wenye uzoefu na michuano ya kimataifa kama
Fabrice Ngoma kutoka Al Hilal ya Sudan, Luis Miqquisone kutoka Al Ahly, Willy Onana
aliyekuwa akikipiga Rwanda, Aubim Kramo kutoka Asec Mimosas, Shaban Chilunda na wengine wengi.

Usajili huo umeanza kulipa kwa sababu wengi wameonesha wao ni wakali katika michezo
kadhaa iliyopita. Kwenye ligi wameshinda michezo yote miwili wakiwa na pointi sita ila safu ya ulinzi tangu kuumia kwa beki wao tegemeo Henock Inonga inaonekana kupwaya baada ya kuruhusu mabao mawili kwenye nyavu zao.

Waliopo sio kwamba ni wabaya isipokuwa huenda hawaendani na kasi au pengine ni mazoea. Mchezo wa kwanza Simba iliifunga Mtibwa Sugar mabao 4-2 kisha wa pili ikaifunga Dodoma Jiji mabao 2-0.

Ndio mabingwa wa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti
kufuatia kutoka suluhu dakika 90 za mchezo huo.

Simba wanaonekana wako makini wanataka kuendelea kufanya vizuri kwenye ligi lakini zaidi malengo yao wanatazama michuano miwili mikubwa Afrika yaani African Football League (AFL) wanataka kufika mbali zaidi.

Related Articles

Back to top button