
DAR ES SALAAM: KIKOSI cha Yanga kimepata ahueni baada ya baadhi ya wachezaji waliokuwa nje kutokana na majeraha kurejea mazoezini, hatua inayoongeza nguvu kuelekea michezo ijayo ya mashindano mbalimbali.
Wachezaji waliorejea rasmi mazoezini ni Laurindo Aurelio ‘Depu’, Ibrahim Bacca na Chadrack Boka, ambao kwa nyakati tofauti walikuwa nje ya uwanja wakikabiliwa na changamoto za kiafya.
Kurejea kwa nyota hao kunatajwa kuwa habari njema kwa benchi la ufundi la Yanga, hasa katika kipindi hiki ambacho timu hiyo inaendelea kupambana kutetea ubingwa na kufanya vizuri katika mashindano mengine inayoshiriki.
Mbali na wachezaji hao, pia wapo mastaa wengine ambao bado hawajaonekana wakicheza msimu huu lakini wamekuwa wakionekana katika mazoezi ya timu hiyo, akiwemo Abubakar Salum ‘Sureboy’ pamoja na Farid Mussa.
Kutokana na kuendelea kushiriki mazoezi, kuna uwezekano wa wawili hao kurejea kikosini katika mechi zijazo endapo watakuwa wamefikia utimamu wa kutosha wa kimchezo na kiafya.
Hatua hiyo inaweza kuwa nyongeza muhimu kwa kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, ambaye huenda akapata chaguo zaidi la wachezaji katika eneo la ushambuliaji na kiungo kadri ratiba ya ligi na mashindano mengine inavyozidi kushika kasi.




