Kwingineko

Italia yapigwa tena, yashindwa kufuzu Kombe la Dunia

ZENICA, Bosnia na Herzegovina: Italia imeendelea kuandamwa na jinamizi la kutofuzu Kombe la Dunia baada ya usiku wa kuamkia leo kuchapwa kwa penalti 4-1 na Bosnia na Herzegovina kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa mchujo wa kufuzu fainali hizo.

Matokeo hayo yanaifanya Italia, mabingwa mara nne wa dunia, kukosa nafasi ya kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo, jambo linalozidi kuibua maswali kuhusu hali ya soka la taifa hilo kubwa barani Ulaya.

Italia ilianza mchezo huo kwa kasi na kupata bao la kuongoza mapema dakika ya 15 kupitia kwa Moise Kean, lakini matumaini yao yalianza kuyeyuka baada ya beki Alessandro Bastoni kuonyeshwa kadi nyekundu dakika tatu kabla ya mapumziko.

Bosnia ilitumia vyema faida ya kucheza dhidi ya wachezaji 10 na kusawazisha dakika ya 79 kupitia kwa Haris Tabakovic, kabla ya mchezo kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti baada ya dakika za kawaida na za nyongeza kumalizika kwa sare.

Katika mikwaju hiyo, Italia iliporomoka baada ya Pio Esposito na Bryan Cristante kukosa penalti zao, huku Bosnia ikipiga kwa umakini na kufanikiwa kushinda kwa jumla ya penalti 4-1.

Ushindi huo unaifanya Bosnia kufuzu Kombe la Dunia na kutinga Kundi B, ambako itakutana na wenyeji wenza Canada, pamoja na Qatar na Switzerland.

Kocha wa Bosnia, Sergej Barbarez, amesema wachezaji wake wameonyesha uimara mkubwa wa kisaikolojia na kupambana hadi mwisho.

“Vijana hawa wana tabia ya kipekee na tulijua watatufanya tujivunie.
Hawana hofu, wanaingia uwanjani wakiwa watulivu sana,” amesema Barbarez.

Kwa Bosnia, ushindi huo ni wa kihistoria na wa kufuta maumivu ya kushindwa kufuzu katika hatua mbalimbali za mchujo kwa miaka ya nyuma, huku kwa Italia ukiwa ni mwendelezo wa anguko kubwa la soka lao la kimataifa tangu walipotwaa ubingwa wa dunia mwaka 2006.

Tangu ushindi huo wa mwaka 2006, Italia imekuwa na rekodi mbaya kwenye Kombe la Dunia, ambapo ushindi wao pekee katika fainali tangu wakati huo ulikuwa mwaka 2014.

Kwa upande wa Bosnia, kijana Kerim Alajbegovic mwenye umri wa miaka 18 aliendelea kuonesha ujasiri mkubwa baada ya kufunga moja ya penalti muhimu dhidi ya Italia, akithibitisha nafasi yake kama mmoja wa nyota wanaochipukia wa timu hiyo.

Related Articles

Back to top button