Olympique Lyon, Nice yamewakuta!
Kamati ya nidhamu ya Ligue 1 ya Ufaransa (Ligue de Football Professionnel) LFP imeziadhibu klabu za Olympique Lyon na Nice zinazoshiriki ligi hiyo kufungwa kwa sehemu ya viwanja vyao kufuatia vurugu za mashabiki walizofanya katika michezo yao ya mapema mwezi huu.
Mashabiki wa Lyon walitumia mafataki katika mchezo ambao walishinda kwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya St Etienne mapema mwezi huu, huku wafuasi wa Nice pia wakiachia vifaa hivyo kwenye sare ya 2-2 na wageni Lille matendo ambayo yaliingilia na kusimamisha mchezo kwa muda.
Mambo haya si mageni kwa mashabiki wa soka la Ufaransa, ikumbukwe kuwa Nantes waliwahi kufungiwa uwanja kwa mechi moja baada ya mashabiki wao kurusha vitu kwenye ‘pitch’ na kujaribu kuvamia uwanja walipopoteza 2-0 nyumbani mbele ya Le Havre siku ya Jumapili na LFP, wanachunguza tukio hilo, na uamuzi ni Desemba 18.
Olympique Marseille pia walipewa adhabu kama hiyo baada ya watazamaji kurusha vitu walipotandikwa 3-1 nyumbani na AJ Auxerre mwezi huu.
Lyon iliyo katika hatari ya kushushwa daraja kutokana na madai ya ubadhirifu wa fedha ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligue 1, na itakuwa mwenyeji wa Nice inayoshika nafasi ya tano wikiendi hii.