Singida BS, Azam FC hapatoshi

SINGIDA: SINGIDA Black Stars inatarajiwa kushuka dimbani kesho kuikabili Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa kwenye Uwanja wa Airtel, mkoani Singida.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia ya timu hizo mbili pamoja na nafasi zao kwenye msimamo wa ligi.
Takwimu zinaonesha kuwa katika michezo 10 ya mwisho ambayo timu hizo zimekutana, Azam FC imeibuka na ushindi mara sita, huku Singida Black Stars ikishinda michezo miwili na timu hizo kutoka sare mara mbili.
Kwa sasa, Azam FC ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 29, wakati Singida Black Stars inashika nafasi ya sita kwa pointi 25, hali inayoongeza uzito wa pambano hilo kwa kila upande kutaka kujiimarisha zaidi.
Akizungumzia mchezo huo, Msemaji wa Singida Black Stars, Hussein Masanza, amesema wanafahamu ubora wa wapinzani wao, lakini wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri mbele ya mashabiki wao.
Amesema maandalizi ya timu hiyo yamekamilika na morali ya wachezaji ipo juu kuelekea mchezo huo muhimu wa kusaka pointi tatu.




